21 August 2012



SENSA ya watu na makazi inatarajia kufanyika nchini kuanzia usiku wa kuamkia Agosti 26 mwaka huu na itafanyika kwa siku saba.

Lengo la Serikali ni kuhakikisha watu wote wanahesabiwa ili kupata taarifa ambazo zitasaidia kupanga, kufanya maamuzi, kusimamia na kutathmini sera na mipango ya maendeleo.

Taarifa za sensa pia hutumiwa na sekta binafsi katika shughuli za kila siku hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi, kushiriki ili kuipa nadasi Serikali ifahamu mahitaji ya kila Mtanzania.

Kabla ya kuanza mchakato huo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeanza kutoa mafunzo kwa makarani wa sensa katika mikoa yote nchini ambao watahusika kuhesabu watu.

Takwimu ambazo zitakusanywa, zitatumika kutunga sera za kiuchumi, kijamii na kutathamini hali ya maisha ya wananchi hivyo ni wazi kuwa, sensa hii imeweka mkazo mkubwa katika maendeleo.

Hivi karibuni, vyombo vya habari vimeripiti migogoro iliyopo kwa baadhi ya makarani wanaoshiriki mafunzo hayo na kubwa zaidi ni wahusika kutopewa stahiki zao (posho), za kushiriki mafunzo hayo.

Katika baadhi ya maeneo, vurugu kubwa zimetokea sambamba na makarani kususia mafunzo waliyokuwa wakipewa na wakufunzi wakitaka NBS iwalipe fedha zao ili waendelee na mafunzo.

Sisi tunasema kuwa, upo umuhimu mkubwa wa NBS kurekebisha kasoro zilizopo hasa kwa makarani hao ili Sensa ya Watu na Makazi iweze kufanikiwa kama ilivyopangwa.

Baadhi ya makarani wanasema pamoja na kushiriki mafunzo siku tano mfululizo, dalili za kupata posho zao hawazioni na hakuna majibu ya kulidhisha ambayo wanayapata kutoka kwa wahusika.

Wengine wanadai pamoja na kushiriki mafunzo siku tatu hadi nne na kutolipwa posho zao, majina yao yamekatwa kwa maagizo ya viongozi wanaotoa (vimemo) na kupachika ndugu zao

Tuhuma hizi kama zina ukweli wowote, zinaitia doa NBS ambayo ndio iliyopewa jukumu la kuratibu mchakato huu ambao hivi sasa, viongozi mbalimbali wa kisiasa na dini, wanatumia fursa walizonazo kuhamasisha wananchi waone umuhimu wa kuhesabiwa.

Upo uwezekano wa makarani ambao hivi sasa wamejenga chuki na NBS, kuharibu mchakato huo ili kuikomoa Serikali jambo ambalo linaweza kupotosha ukweli wa idadi kamili ya Watanzania ambao wamefikiwa na makarani husika ili kuhesabiwa.

Pamoja na changamoto zilizopo, kila mwananchi ajiandae kuhesabiwa na kujibu maswali ambayo wataulizwa na makarani ili lengo la sensa litafanikiwa kama inavyotarajiwa.

No comments:

Post a Comment