16 January 2013

Mtemvu atoa ushauri kwa Mahakama




Na David John

MBUNGE wa Temeke, Dar es Salaam, Bw. Abbas Mtemvu, amezishauri mahakama nchini kuharakisha usikilizaji wa kesi
za watu waliojenga na kuzuia mifereji ya maji machafu.

Alisema kesi hizo zinapochelewa kutolewa hukumu, zinachangia kukwamisha maendeleo kwenye mitaa ya kata mbalimbali ambapo hali hiyo ndiyo iliyojitokeza katika jimbo hilo.

Bw. Mtemvu aliyasema hayo Dar es Salaam juzi wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usafi wa Mazingira uliofanyika kwenye Kata ya Makangarawe, eneo la Yombo jimboni humo.

“Naziomba mahakama zote nchini ziharakishe kutoa hukumu ya
kesi zilizofunguliwa na wananchi kuweka pingamizi la kuzuia mifereji au mikondo ya maji machafu isipite eneo fulani au
katika kata zao.

“Umefika wakati wa mahakama kuunga mkono jitihada ambazo zinafanywa na Serikali hasa katika kuboresha miundombinu ya mazingira ili kuharakisha maendeleo ya jamii,” alisema.

Aliongeza kuwa, changamoto zinazokwamisha masuala ya usafi hasa wa mifereji ya maji machafu ni kesi zinazofunguliwa na wananchi kupinga upitishaji mfereji katika eneo la nyumba yake mbali ya kupewa notisi ya kuondoka lakini hawataki,” alisema.

“Kwa mfano, kundi linaloitwa MEG limejitolea kufanya usafi wa mazingira katika Kata ya Makangarawe lakini kuna mwananchi mmoja amekwenda kuweka pingamizi mahamani kuzuia mfereji
wa maji machafu usipite sehemu ya nyumba yake.

“Mbaya zaidi huyu mwananchi ameshalipwa fedha nyingi na Serikali zaidi ya sh. milioni 220 ili aweze kuhama eneo husika
kupisha ujenzi wa Barabara Kuu ambayo ipo chini ya Wakala
wa Barabara nchini (TANROADS),” alisema.

Bw. Mtemvu alisema, jambo la kushangaza mbali ya kupata fedha hizo bado hataki kuondoka na hivi sasa anazuia mfereji wa maji machafu usipite katika eneo lake.

Akizungumzia changamoto ya kusafisha mazingira katika kata hiyo, Bw. Mtemvu aliwataka wananchi kuunga mkono jitihada ambazo zinafanywa na Kundi la Makangarawe Enveromental Group (MEG), kwa kufanya usafi wa mazingira na jukumu hilo si la kwao pekee.

Katika uzinduzi huo, Bw. Mtemvu alichangia zaidi sh. 300,000 ili kundi hilo liendelee kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi na kuahidi kuzungumza na Serikali Mkoa ili wapewe kazi ya kusafisha barabara ya Yombo kutokana na nia yao ya kutaka kata hiyo iwe ya mfano.

Katika hatua nyingine diwani wa kata hiyo, Bw. Victor Mwakasendile, alilipongeza kundi hilo na kuahidi kushughulikia suala la dampo ili uchafu wote unaokusanywa ukatupwe huko.

No comments:

Post a Comment