14 January 2013

Mbunge atoa msaada wa shuka za mil. 17.5/-


Na Mwandishi Wetu, Geita

MBUNGE Viti Maalumu, mkoani Geita, Bi. Josephine Chagula (CCM), ametoa msaada wa shuka 400, kwa Hospitali za Wilaya
mkoani humo, zenye thamani ya sh. milioni 17.5, kwa ajili ya
wanawake wajawajito waliolazwa katika hospitalini hizo.


Msaada huo umetolewa juzi kwa hospitalini Wilaya ya Geita, Chato, Mbogwe na Nyang'hwale ambapo kila hospitali imepata shuka 100 kwa ajili ya matumizi ya wodi za wazazi.

Akizungumza wakati akitoa msaada huo, Bi. Chagula alisema utasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa shuka kwani wanawake wengi hutaabika wakati wa kujifungua.

“Wanawake ambao wanajifungua katika hospitali zetu, mara nyingi hukosa vifaa muhimu kama shuka...nimeguswa na tatizo hili ndio maana nikaamua kutoa msaada huu,” alisema.

Aliongeza kuwa, msaada huo umelenga kutoa changamoto kwa wadau wengine wakiwemo viongozi wa Serikali, vyama vya siasa
na taasisi za dini zenye uchungu na matatizo waliyonayo wanawake ili wajitokeze na kutoa misaada ambayo itasukuma mbele maendeleo katika sekta ya afya nchini.

Bi. Chagula alishhudia vitanda vingi katika wodi wazai kwenye Hospitali ya Geita, Chato na Bukombe vikiwa havina shuka na magodoro yake yakiwa yamechakaa.

Akimpongeza mbunge huyo kwa msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Bi. Lilian Matinga, alisema hospitali hiyo ilikuwa ikikabiliwa na tatizo kubwa la shuka hivyo msaada huo umetolewa kwa wakati muafaka.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, alimtaka Bi. Chagula anapozungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara, atumie fursa hiyo kuhimiza umuhimu wa afya, ujenzi wa nyumba bora na imara za kuishi.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, alisema juhudi za Bi. Chagula zinapaswa kuungwa mkono na wabunge wenzake mkoani humo katika kuboresha mazingira ya sekta ya afya ambayo  inayowagusa wananchi wengi.

Baadhi ya madaktari wa hospitali hizo, walimpongeza Bi. Chagula kwa msaada aliotoa na kumuomba ashughulikie tatizo la upungufu wa watumishi wakiwemo wauguzi na madaktari, upatikanaji wa mashine za kufulia, dawa na kuboresha vyumba vya kuhifadhi
maiti ambavyo vinahitaji ukarabati mkubwa.

No comments:

Post a Comment