14 January 2013

Slaa kuanza ziara ya kichama K'njaro leo


Na Martha Fataely, Moshi

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Slaa, anatarajiwa kufanya ziara
ya siku mbili mkoani Kilimanjaro kuanzia leo kwa ajili ya
kuelezea mafaniko ya chama na shughuli za mwaka 2013.


Katibu wa chama hicho mkoani humo, Bw. Bazil Lema, alisema Dk. Slaa atafanya ziara katika Wilaya za Moshi, Same pamoja na kutoa ufafanuzi wa matukio yaliyotokea 2012.

Akizungumza kwa niaba ya Bw. Lema, Mwenyekiti wa Madiwani
Manispaa ya Moshi, Bw. Jomba Koyi, alisema Dk. Slaa atafungua matawi katika Kata za Karanga, Longuo, Nfumuni, Majengo, Mawenzi Bondeni, Njoro pamoja na Ofisi ya Kata.

“Pia Dkt. Slaa atafanya mkutano wa hadhara saa nane mchana eneo la Stesheni ya Reli ambapo pamoja na mambo mengine, atatoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania,” alisema.

Aliongeza kuwa, katika ziara hiyo Dkt. Slaa atazungumzia mikakati ya chama kwa mwaka 2013, kuelezea mafaniko na changamoto za chama kwa mwaka ulioisha pamoja na kutoa ufafanuzi wa matukio yaliyotokea ndani ya chama mwaka 2012.

“Miongoni mwa mambo ambayo atayatolea ufafanuzi ni pamoja na shughuli za chama zilizofanyika mwaka 2012 ukiwemo uanzishwaji wa Mikutano ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C),” alisema.

Bw. Koyi alisema akiwa wilayani Same, Dkt. Slaa ambaye ataongozana na viongozi wengine ndani ya chama hicho,
 atafungua matawi katika kata nne za Same mjini, Makanya,
Suji, Hedaru pamoja na kutafanya mkutano wa hadhara.

No comments:

Post a Comment