22 January 2013

Makamba afumua menejimenti TTCL



Na Mariam Mziwanda

NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ameahidi kufumua uongozi uliopo katika Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kutokana na shutuma za ubadhirifu yakiwemo matumizi mabaya ya uongozi.


Makamba aliyasema hayo Dar es Salaam jana mara baada ya kupokea ripoti kutoka kwa wafanyakazi wa shirika hilo zilizoeleza vitendo viovu vinavyofanywa na viongozi wa shirika katika kuhujumu mali za umma.

Alisema kuwa, mbali na mikakati ya Serikali iliyopo kulipatia viongozi madhubuti shirika hilo pia amewasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuwachukulia hatua viongozi wanaohusika na ubadhirifu huo.

"Mimi kama raia na kiongozi nimetoa taarifa TAKUKURU tayari, imekua bahati kwangu leo nimepokea ripoti za wafanyakazi ambazo zina vielelezo vya kutosha juu ya tuhuma za viongozi ambao ni wabadhirifu na wana matumizi mabaya ya uongozi hii itarahisisha zaidi uchunguzi na sheria kuweza kutumika,"alisema.

Aliongeza kuwa, juhudi hizo zitakwenda sambamba na kuhakikisha hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamni viongozi hao zinafikiwa hivyo amewataka wafanyakazi wengine wenye vielelezo waunge mkono kwa maslahi ya taifa.

Makamba alidai kusikitishwa na udhaifu wa uongozi uliopo katika shirika hilo ambao unajieleza kuwa hakuna heshima wala staha ya shirika hivyo kufananisha mfumo wa kazi baina ya viongozi na watumishi kuwa sawa na makuli bandarini.

Alisema, Serikali ina wajibu wa kuona shirika hilo linarudi katika mfumo bora wa mashirika ya umma hivyo ni lazima mabadiliko hayo ya uongozi yaende sambamba na nafasi hizo kutangazwa ili kupata uongozi wenye sifa na imara hatimaye shirika liweze kurudisha hadhi na kuaminika.

"Kwa hali iliyopo sasa shirika ni baya na imefikia sasa haliwezi hata kukopesheka, hivyo tunatambua mtaji uliopo ni mdogo.

"Lakini kwa harufu ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya uongozi tumesitisha hata kutoa dhamana mpaka pale litakapokaa sawa na kuweza kuamika ili liweze kukopesheka," alisema Makamba.

Alisema, mabadiliko hayo yatakwenda sambamba na Serikali kulitoa shirika hilo katika ubia na Kampuni ya Airtel ili kuongeza nguvu ya ufanisi na uhuru wa maslahi ya shirika hilo.

Makamba alieleza harakati hizo za kuondokana na ushiriki wa Airtel katika ubia na TTCL zinasubiri maamuzi ya Msajili wa Azina ili kuweza kulipa tathimini ya thamani ya ushiriki.

Pia aliitaka bodi ya shirika hilo kukutana mapema wiki hii na kutoa taarifa kwa CAG ili aweze kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha za shirika huku akiitaka bodi hiyo pia kuhakikisha inawapumzisha viongozi waliopo ili kuruhusu uchunguzi huru.

Makamba alimtaka Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Said Amir Said kuhakikisha hakuna mfanyakazi anayeonewa kwa utendaji wake wa kazi hasa kuwajibishwa kwa kuhamishwa kituo ili kuruhusu ubadhirifu wa mabilioni ya fedha kuendelea.

Pia alielezea kusikitishwa na hali mbaya iliyopo TTCL ya kukosa hata dola 2,000 za kuunganisha wateja huku wizi wa mikonga ya simu na mitambo ukiendelea.

Awali wafanyakazi wa shirika hilo wakiongozwa na Lucas Ishengoma walimueleza Naibu waziri huyo mchezo mchafu uliopo hasa Kanda ya Kaskazini, Dar es Salaam ambapo viongozi wamekuwa wakifanya watakavyo.

"Tunaelewa fika kuwa bajeti ya shirika letu ni sawa na mbwa asiyebweka, kwani inaongozwa na matakawa ya viongozi na sasa hivi kwa kuwa Kanda ya Kaskazini tukiongozwa na meneja tunaonekana tunafuatilia sana mapato na matumizi na tunaonekana tunakiherehere cha utendaji wa kazi.

"Tayari taarifa za meneja kuhamishiwa Mwanza tunazo ili aletwe rafiki wa mabosi, wale vizuri, lakini tunachosema tumechoka huyo mnayemleta hatumtaki kakaeni naye makao makuu,"alisema

Walisema kuwa, wakati uliopo hauna tofauti na ukoloni wa Mwarabu ndani ya shirika hilo kwani kazi ya uongozi ni kupitisha mikataba hewa ambayo haina maslahi kwa taifa huku wakiomba mapato ya mkongo wa taifa wa mawasilaino ambayo hayawafikii.

Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Said Amir Said aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa mabadiliko yoyote yatakayofanywa na Serikali watayapokea hivyo ni vyema mchakato kuanza mapema.

6 comments:

  1. MAKAMBA TATIZO SIO WAFANYAKAZI KAMA BABA NI MWIZI UNATARAJIA NINI DAWA WAKUBWA WAO KUBADIRIKA MBONA WAKATI WA NYERERE HATUKUWA NA MAFISADI BALI WADOKOZI TU SIKU HIZI WIZI NI SYNDICATE KUANZIA CHINI MPAKA JUU NA JUU MPAKA CHINI. NENDA OFISI YEYOTE YA CCM BILA CHOCHOTE HUPATI HUDUMA. KWA MFANO WAKATI KUANDIKISHA RAIA DSM. BILA 3000/= BALOZI CCM HAKUPI BARUA KUKUTAMBULISHA WENYE MISIMAMO HATUKUANDIKISHWA

    ReplyDelete
  2. WATAALAMU WOTE CREAM YA TTCL ILIHAMIA TCRA,VODACOM,TIGO NK KWAHIYO MAZINGIRA MAZURI YAKIWEPO YA MASILAHI WATARUDI.

    ReplyDelete
  3. TATIZO LA WATANZANIA NI KUSHINDWA KUKUBALIANA NA MFUMO WA SOKO HURIA WALILODANDIA BAADA YA KUZIKA AZIMIO LA ARUSHA NA KUANZISHA AZIMIO LA ZANZIBAR KIKO KIAPO KUWA AZIMIO LA ARUSHA HALITAREJESHWA MILELE NDIO SABABU WAZUNGU WAKAWEKEZA NA SI WAZUNGU TU NA WATANZANIA AMBAO LEO WANAITWA MAFISADI[WANAOCHUKUA WAKE ZA WATU]TATIZO BADALA YA UCHUMI HURIA TANZANIA NI UCHUMI HOLELA MTAISHIA UVUVUZELA KENYA INAONGOZA KWA ICT AFRIKA TANZANIA IKIONGOZA KWAUVIVU WA KUFIKIRI NA USHIRIKINA KATIKA DUNIA

    ReplyDelete
    Replies
    1. Wee jamaa uliandika hapa juu January 23, 2013, una akili sana. Unaongea point. Na tuseme Watanzania wachache waliosoma ndio wanapoteza Taifa, maana wengi sana hawajasoma na si kosa lao, maana elimu ni duni kwetu. Lakini hao wachache wanapiga vuvuzela sana.

      Delete
  4. Si kweli kwamba wakati wa Nyerere hakukuwa na matatizo, wala ufisadi. Nyerere hakuwa malaika anye alikuwa na mapungufu yake. Tusiwe kama mataahira

    ReplyDelete
  5. Mhe Makamba, wizi/ufisadi kwenye kampuni ya TTCL ulianza kitambo kidogo na wizi ulianza kwa kasi zaidi 2006 kuna syndicate katika accounting system viongozi wanashirikiana kuchukua fedha. Wengi waadilifu walistaafishwa kabla ya wakati na wengine kuhamishwa na wataalamu wengi waliacha kazi. Financial system ikaguliwe na IT professionals kutoka nje....madudu mengi yapo.

    ReplyDelete