03 January 2013

Makachero wa Polisi wavamia Z'bar *Kuwasaka waliompiga risasi Padri Mkenda


Na Mohammed Mhina, Jeshi la Polisi Zanzibar

JESHI la Polisi Makao Makuu jijini Dar es Salaam, limetuma timu ya makachero kwenda Zanzibar kuungana na wenzao ili kufanya upelelezi wa tukio la kushambuliwa Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mpendae.

Kanisa hilo lipo katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar
ambapo Padri Mkenda alijeruhiwa kwa kupigwa risasi kidevuni
na watu wasiofahamika Desemba 25 mwaka huu, wakati akitoka
kanisani kwenda Hosteli ya Tomondo anayoishi.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar,
ACP Yusuf Ilembo, alisema timu hiyo inaongozwa na Ofisa mmoja
wa ngazi ya juu (bilakumtaja jina), yenye jumla ya makachero watano waliobobea katika masuala ya upelelezi nchini.

Alisema lengo la Mkuu wa jeshi hilo nchini, IGP Saidi Mwema, kuituma timu hiyo ni kutaka kuongeza nguvu ya uchunguzi wa
tukio hilo ambalo linatazamwa tofauti hasa kwa kuzingatia kuwa, aliyeshambuliwa ni kiongozi mkubwa wa dini na limetokea katika kipindi cha Sikukuu ya Krismasi.

“Jeshi la Polisi Makao Makuu Dar es Salaam limeamua kufanya upelelezi wa tukio hili kwa ushirikiano wa pamoja na makachero waliopo Zanzibar ili kuhakikisha wote waliohusika kumshambulia Padri Mkenda wanakamatwa,” alisema.

Kamanda Ilembo aliongeza kuwa, bado wanaendelea na uchunguzi kubaini sababu za kushambuliwa Padri Mkenda huyo na kumjeruhi bila kuchukua kitu chochote.

“Inawezekana watuhumiwa walishindwa kuchukua kitu chochote baada ya kubaini kuwa eneo la tukio lisingekuwa salama kwao
kwa vile kulikuwa na walinzi karibu,” alisema.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar,
ACP Aziz Juma Mohammed, amewatahadharisha wazazi na
walezi kutowaruhusu watoto wao kurandaranda barabarani
au kwenda katika fukwe za bahari kuogelea bila uangalizi
wa watu wazima.

Alisema uzoefu unaonesha kuwa, watoto wengi wamekuwa wakigongwa na magari au kuzama na kufa maji kutokana na
kukosa uangalizi wa watu wazima.

Wakati huo huo, Mwandishi Gladness Theonest anaripoti kuwa,
Padri Mkenda ambaye hivi sasa amelazwa katika Taasisi ya Tiba
ya Mifupa (MOI), iliyopo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana alifanyiwa upasuaji wa kutolewa risasi.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Ofisa Habari wa MOI Bw. Almas Jumaa, alisema hali ya Padri huyo inaendelea vizuri.

No comments:

Post a Comment