03 January 2013
Kesi ya Dkt. Namala Mkopi kusikilizwa Januari 23
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imepanga kuanza kusikiliza kesi inayomkabili Rais wa Chama cha Madaktari
nchini (MAT), Dkt. Namala Mkopi, Januari 23 mwakani.
Wakili wa Serikali Bi. Lucy Diganyeki, mbele ya Hakimu Hellen Liwa, aliieleza Mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeletwa jana kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Katika kesi hiyo, Dkt. Mkopi anakabiliwa na mashtaka mawili, likiwemo la kutotii amri ya Mahakama ya kuzuia mgomo wa madaktari na kuhamasisha mgomo kinyume cha sheria.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, akisaidiana na Ladslaus Komanya,
ulidai kati ya Juni 26 na 28 mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa Rais wa MAT, hakutii amri iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Kazi, Juni 26
mwaka huu.
Ilidaiwa kuwa, amri hiyo ilimtaka Dkt. Mkopi kuwatangazia wanachama wake kuwa wamezuiwa kushiriki mgomo.
Shitaka la pili, inadaiwa Juni 27 mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa mjumbe wa MAT, aliwashawishi wajumbe wa chama hicho kufanya mgomo kinyume cha amri iliyotolewa
na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi, Juni 22 mwaka huu.
Mshitakiwa huyo anatetewa na jopo la mawakili wanne, likiongozwa na Isaya Matamba, Dkt. Maulid Kikondo, Dkt. Gaston Kennedy na Dkt. Rugemeleza Nshala.
Dkt. Mkopi yupo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya dhamana sh. 500,000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment