15 January 2013
Mafunzo kwa waendesha pikipiki yatapunguza ongezeko la ajali
HIVI karibuni, usafiri wa pikipiki mijini na vijijini katika mikoa mbalimbali nchini, umeongezeka kwa kasi kubwa.
Tofauti na siku za nyuma, hivi sasa barabara nyingi katika miji mikubwa ukiwemo Dar es Salaam, zimetapakaa vyombo hivyo ambavyo siku za nyuma viliogopwa kwa hofu ya ajali.
Kuna mambo mengi ambayo yamesababisha ongezeko la vyombo hivyo hasa kufunguliwa kwa milango ya biashara ambako kumechangia pikipiki nyingi kuletwa nchini.
Leo hii maduka mbalimbali hasa yaliyopo katikati ya miji,yanauza pikipiki kama njugu na bei zake ni nafuu ukilinganisha na miaka iliyopita.
Usafiri huu umeonekana kuwa na tija kwa watu wengi hasa kukwepa foleni kubwa za magari na kuwahi maeneo mbalimbali.
Vijana wengi wameamua kujiajiri kupitia vyombo hivyo kwa kusafirisha abiria kama ilivyo kwa nchi jirani ya Uganda ambayo muda mrefu, pikipiki maarufu kama 'bodaboda' ni usafiri muhimu.
Pamoja na wepesi wa usafiri huu, upo umuhimu mkubwa wa Jeshi la Polisi na wadau wengine kutoa elimu kwa waendesha pikipiki hasa zinazofanya biashara ya kubeba abiria ili kuhakikisha watumiaji wa vyombo hivyo na abiria wanakuwa salama.
Katika Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine nchini, kila siku waendesha pikipiki wanapata ajali wengine wakipoteza maisha
au kupata vilema vya kudumu.
Kwa kiasi kikubwa matatizo haya yanachangiwa na watumiaji wengi wa vyombo hivi kutokuwa na ujuzi wa kuvitumia na kutofahamu sheria za usalama barabarani. Wengi wanaendesha kwa uzoefu bila kufuata sheria husika.
Ukweli ni kwamba, asilimia kubwa ya waendesha pikipiki hawana leseni zinazowaruhusu kutumia vyombo hivyo. Ili kuzuia ajali nyingi zinazotokea kila siku, umefika wakati wa Jeshi la Polisi
na wadau wengine kuendelea kutoa mafunzo bila kikomo kuhusu namna ya kutumia barabara ili kuokoa maisha yao.
Mafunzo hayo yatawasaidia kujenga uelewa kwa waendesha pikipiki kupunguza ajali zinazotokana na usafiri huo.
Hiyo ndio njia pekee ambayo itasaidia kuokoa maisha yao na abiria.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment