14 January 2013

Tupinge mauaji ya raia wasio na hatia kulinda amani nchini


Na Daniel Samson

HAKI za binadamu ni moja ya mambo muhimu ambayo sheria na taasisi za kimataifa za haki za binadamu zinasisitiza kuwepo kwa usawa na haki miongoni mwa watu wa jamii mbalimbali.

Suala hili linatekelezwa kwa mitazamo tofauti na watawala katika nchi mbalimbali kutokana na mfumo wa sheria unaoongoza nchi.


Kuishi ni moja ya haki za msingi ambazo binadamu anatakiwa kupata ili apate stahili nyingine akiwa hai.

Neno haki za binadamu ni muunganiko wa maneno mawili haki na binadamu, ambapo haki ni stahili alizonazo mtu na anatakiwa azipate kumwezesha kuishi.

Wapo binadamu na wasio na utu kwa sababu binadamu ni dhana ya kiitikadi ambayo humtambulisha mtu na stahili muhimu alizonazo katika maisha ya kila siku. Ikiwa mtu hana sifa ya kuwa binadamu basi hana stahili muhimu zinazomwezesha kuishi katika mazingira yanayomzunguka.

Ni dhana ya kihistoria ambayo hutengeneza matabaka mawili ambayo huwa na uhasimu mkubwa kwa kila kundi kupigania haki za msingi za kuishi katika mazingira mazuri.

Katika mfumo wa ujamaa/ujima watu katika jamii bila kujali matabaka ya uongozi, umri na jinsia humiliki rasilimali zinazowazunguka kwa usawa na haki bila kubaguliwa na kunyanyaswa.

Tabaka la wenye kutumia rasilimali zaidi ya wengine halina nafasi katika mfumo huu. Na jamii nyingi zimejaribu kuishi kwa kutumia mfumo huu lakini imekuwa vigumu kuutimiza kwa kuwa binadamu tunazaliwa tofauti katika tabia na mitazamo lakini tunaunganishwa kwa maadili yaliyopo katika jamii.

Mfumo mwingine wa maisha wa kikabaila huimiza umiliki wa  rasilimali za jamii kuwa katika mikono ya watu wachache ambao hutumia utajiri wa nchi kwa manufaa yao binafsi, lakini kundi linalobaki ambalo hujumuisha watu wengi ambao humiliki sehemu ndogo ya rasilimali za jamii na hawanufaiki na utajiri wa nchi.

Mfumo huu wa kisiasa ndio unaotumika kuongoza mataifa mengi duniani ikiwemo Tanzania yenye mfumo wa kijamaa lakini inatekeleza sera za mabepari ambazo zina matabaka mawili ya wenyenacho na wasionacho.

Kundi la wenyenacho ama matajiri ndilo lina nguvu kubwa ya kisiasa na kiuchumi ambapo hutumia mamlaka hiyo kunyanyasa na kuwanyonya maskini.

Maskini ndio hukumbwa na matatizo makubwa wakitaka kupigania haki zao katika jamii kwa kupata vitisho na upinzani kutoka katika kundi la binadamu ambao hawataki kuguswa katika maslahi yao.

Matukio mbalimbali ya mauaji ya raia wasio na hatia  yanayotokea katika nchi yetu ni ishara tosha kuwa kuna binadamu na wengine wasio binadamu.

Miaka minne iliyopita tumeshuhudia mauaji yaliyotekelezwa na askari polisi ambapo watu wengi wamekuwa wakipigwa risasi kwa sababu mbalimbali ikiwemo uhalifu unaotokea katika maeneo ya nchi yetu.

Matukio ya mauaji hupangwa ama hufaywa bila kukusudiwa ili kutimiza matakwa ya kisiasa ya watu wachache katika jamii ambao kila wanapoguswa katika maslahi yasiyo na manufaa katika maendeleo ya nchi hutumia vyombo vya dola kuwadhuru na kuwatisha walalahoi.

Uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) unaonyesha takwimu za mauaji ya raia wasio na hatia zinaongezeka kila mwaka ambapo katika kipindi kifupi cha kuanzia Januari mwaka, jana  watu waliouawa kwa kupigwa risasi ni 22.

Idadi hii ni kubwa kwa nchi kama Tanzania ambayo ina historia ya kuwa na amani muda mrefu na mauaji haya yanatekelezwa na polisi ambao ndio wanaowajibika kuwalinda wananchi lakini ikiwa tumefikia hatua hii ya kuua raia kwa sababu ambazo hazina msingi wowote tunatabiri hali tete kwa mustakabali wa Taifa.

Uchunguzi huu unatoa tena takwimu nyingine za mwaka 2007 ambapo watu 14 walipigwa risasi na kuuawa. Kutokana na wanaharakati wa haki za binadamu kupinga mauaji holela ya raia idadi hiyo ilipungua na kufikia watu 8 mwaka 2008.

Sababu mbalimbali zimekuwa zikitolewa na polisi kuwa mauaji haya hutokea hasa kwa wahalifu ambao hukataa kusalimu amri wakati wa mapambano ya kurushiana risasi wakati wa matukio ya uhalifu.

Pia katika mwaka huohuo takwimu zinaonyesha watu 15 walifariki kwa kupigwa risasi, idadi iliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2008 ambapo walifariki watu 8.

Hatukatai polisi kuwadhibiti wahalifu kwa risasi lakini idadi hii ya mauaji ya raia wasio na hatia ambao wanashiriki katika mikutano ya kisiasa au wanapinga mfumo dharimu wa kinyonyaji ambao unawachukulia watu wengine kama wanyama na sio binadamu na hivyo hata wakipigwa risasi na kufariki inachukuliwa ni jambo la kawaida.

Mwaka 2011 idadi iliongezeka na kufikia vifo 25 ikilinganishwa na mwaka 2009 ambapo waliouawa ni 15.

Vifo hivi ni sehemu ya vurugu zilizotokea mkoani Arusha ambapo wafuasi wa CHADEMA walipambana vikali na polisi na watu watatu walipigwa risasi na kufariki dunia.

Mwaka 2012 tangu uanze ni watu 22 wamepigwa risasi na polisi akiwemo mtu mmoja aliyefariki katika maandamano ya wafuasi wa CHADEMA mkoani Morogoro.

Polisi hawakuishia hapo safari hii wakatekeleza mauaji kwa raia ambaye ni mwandishi wa habari Daud Mwangosi ambaye aliuawa kwa bomu ambalo liliharibu mwili wake kiasi cha kutotambulika. Mauaji haya yaliliacha taifa katika hofu na majonzi makubwa kwa sababu kifo hiki kilikuwa ni cha kinyama kwa binadamu.

Najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu, labda askari wetu wameona kutumia risasi hakutimizi hatma yao kuwaondolea uhai watu wasio binadamu kwa sababu mtu huyu akiishi au asipoishi hana maana katika jamii na wameanza kutumia mabomu ili kuendeleza vitisho kwa raia.

Pamoja na yote haya wengi watafikiri kazi ya askari polisi ni kutumia nguvu kubwa kuwadhibiti raia na isipowezekana kutumia risasi za moto lakini jukumu la askari ni kuwalinda raia na mali zao, kuwatambua wahalifu na sio kuwaua. Kwa matukio haya ujiulize upo katika kundi lipi?

Haya yote ni matokeo ya mfumo wa kuongoza nchi ambao hautoi haki sawa kwa raia wote bila kujali matabaka ya kidini na kikabila. Mfumo uliopo unapendelea na kulinda zaidi maslahi ya watawala.

Hili limejidhihirisha katika jumuia za kimataifa zinazohusika na haki za binadamu ambapo Tanzania inatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi tano duniani zenye mfumo mbovu wa sheria unaosimamia haki za binadamu.

Mabadiliko makubwa yanahitajika katika mfumo wa sheria ili kubainisha wazi nani ni binadamu na asipopata haki zake za msingi kama kuishi nani atawajibika.

Jukumu la kulinda haki za binadamu ni la watu wote katika jamii bila kujali tofauti za kidini na kikabila watu walizonazo. Taifa likishindwa kulinda haki za wananchi, jumuiya za kimataifa hazitashindwa kutetea na kulinda haki za binadamu.

Mwandishi ni mwanafunzi wa  shule kuu ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma Chuo Kikuu Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu: 0765299689.



No comments:

Post a Comment