15 January 2013

JK: Mapinduzi Z’bar yamefungua fursa ya elimu kwa WazanzibariNa Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS Jakaya Kikwete amesema, miongoni mwa faida ambazo zimetokana na Mapinduzi ya Zanzibar ni kupatikana kwa fursa
ya elimu kwa wazawa pamoja na watoto zao.


Alisema sababu kubwa ya Chama cha Afro-Shiraz Party (ASP), kufanya Mapinduzi mwaka 1964 ni kuondoa ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi waliokuwa wanafanyiwa Zanzibari
wazawa kupata huduma mbalimbali za msingi hususan elimu.

Rais Kikwete aliyasema hayo juzi alipotembelea Shule ya Sokondari Mlimani-Matemwe, iliyopo Mkoa wa Kaskazini, Zanzibar kwenye Pwani ya Kaskazini ya Kisiwa cha Unguja.

Aliongeza kuwa, inashangaza kuona baadhi ya watu wanayabeza Mapinduzi hayo wakati yameleta faida kubwa na nyingi kwa wananchi ambao wanazijua na kuziheshimu faida zake.

“Sote tunatambua kuwa, sababu kubwa ya ASP kufanya Mapinduzi mwaka 1964 ni kuondosha ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi waliokuwa wanafanyiwa Wazanzibari wazawa kupata huduma muhimu ikiwepo elimu.

“Idadi ya shule ilikuwa ndogo...kwa makusudi wazawa chache ndio waliobahati kupata elimu, baada ya Mapinduzi shule nyingi zilianza kujengwa na vijana wengi kupata elimu,” alisema Rais Kikwete.


Alisema shule hiyo ina majengo ya kisasa, maabara za masomo ya fikizia, kemia, biolojia na kompyuta...ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 1.8...ni moja ya shule 19 za sekondari zinazojengwa visiwani humo chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Lazima (ZABEIP), unaogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar pamoja na Benki ya Dunia.

“Serikali ya Mapinduzi inatoa dola za Marekani milioni sita na Benki ya Dunia milioni 42 ambazo ni mkopo wenye masharti
nafuu na mradi wenyewe ulianza kutekelezwa Julai 2008 na
unatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.

Rais Kikwete alisema chini ya mradi huo, zinajengwa shule 10 za sekondari zenye kidato cha kwanza hadi sita katika kila Wilaya za Tanzania Visiwani, shule tisa za sekondari zenye kidato cha kwanza hadi cha nne, Chuo kipya cha Ualimu cha William Benjamin Mkapa Kisiwani Pemba na shule sita zinafanyiwa matengenezo makubwa.


No comments:

Post a Comment