15 January 2013

Ajali ya basi yaua saba, yajeruhi 28


Robinson Wangaso na Veronica Modest, Mara

WATU saba wamefariki dunia na wengine 48 kujeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha mabasi mawili yaliyogongana uso kwa uso katika Barabara Kuu ya Mwanza, Kijiji cha Nyatwari, wilayani Bunda, mpakani mwa Mkoa wa Mara na Simiyu.

Ajali hiyo imehusisha basi la Mwanza Coach lenye namba T 756 AWT, ambalo lilikuwa likitokea Musoma kwenda Mwanza na basi la Bestline lenye namba T 535 AJR, ambalo lilikuwa likitoka Mwanza kwenda Tarime.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alisema ajali hiyo imetokea juzi saa 11 jioni ambapo watu sita walifariki papo hapo na mmoja alifariki muda mfupi baada ya
kufikishwa katika Hospitali Teule wilayani Bunda (DDH).

Alisema kati ya majeruhi wa ajali hiyo, 14 hali zao ni mbaya na wanne wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando
jijini Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Majeruhi wengine wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hopitali hiyo Teule ya Wilaya ya Bunda na hali zao zinaendelea vizuri, chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa madereva.

“Katika eneo la ajali, barabara yake ipo katika ukarabati na imekwanguliwa hivyo vumbi ni kubwa...madereva walishindwa kuonana na hatimaye kugongana uso kwa uso,” alisema.

Aliongeza kuwa, katika ajali hiyo wanaume waliojeruhiwa ni 27 na wanaume 20 ambapo miili ya marehemu imehifadhiwa kwa ajili ya
utambuzi wa ndugu zao katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda.

Baadhi ya abiria walikuwemo katika mabasi hayo, walisema pamoja na kupiga kelele za kulalmikia mwendo kasi, kilio chao hakikuweza kusikilizwa na baada ya muda mfupi ajali ikatokea.

“Umefika wakati wa Serikali kuchukua hatua kali kwa madereva wazembe ili kuokoa maisha ya abiria wasioa na hatia ambao ni nguvu kazi ya Taifa,” walisema abiria hao.

Wametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuweka askari katika maeneo ambayo mbali kidogo na mji kwani hivi sasa wanakaa katika maeneo ya mijini ambayo madereva wanayafahamu hivyo
kupunguza mwendo ili waonekane wanazingatia sheria.

No comments:

Post a Comment