14 January 2013

Diwani Kwadelo awataka vijana kujikita katika Kilimo Kwanza


Na Charles Lucas

DIWANI wa Kata ya Kwadelo Alhaj Omar Kariati ambaye pia ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amewataka vijana nchini kujikita katika kilimo ili waweze kuondokana na umaskini.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa ajira kwa vijana kupitia Kilimo Kwanza diwani huyo alisema pamoja na kuwa mpango unajulikana nchini, lakini ni vyema vijana wakahamasishwa kushiriki katika kilimo cha kisasa kwa kutumia zana bora ili kujiletea maendeleo.

Bw.Kariati alisema vijana wengi wamekuwa wakikaa vijiweni mijini na vijijini ilhali kuna maeneo makubwa ya kuendeleza kilimo kukuza uchumi wao binafsi na hata kuiondolea serikali mzigo mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana.

Diwani huyo pia alizindua shamba la mfano lenye hekari 40 ambalo litakabidhiwa kwa kikundi cha vijana, ambapo inategemewa itatoa magunia 400 na endapo watapata soko zuri la kuuza mazao yao watapata zaidi ya sh. milioni 40 hivyo wataondokana na adha ya umaskini na kuinua maisha yao.

"Wajibu wetu sisi viongozi ni kuwahamasisha vijana wasio na ajira na kuwawezesha na ndio maana Kata hii ya Kwadelo imekuwa ya kwanza kuingiza trekta ndogo za Power Tiller na hatimaye trekta kubwa kama mnavyoziona hapa.

"Hivyo sisi pia tuwe wa mfano kwa wengine nchini kupata maendeleo kupitia kilimo, alisema Kariati na kuongeza kuwa jumla ya trekta 64 zatalima mashamba ya vijana,"alisema.

Pamoja na uzinduzi huo pia aliwatembelea wakazi   waliokumbwa na mafuriko na kuwapatia msaada wa sh. 500,000, zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernald Membe.

Bw. Membe ni mmoja wa wazee wa kijiji cha Kwadelo ambapo aliwaambia kuwa Waziri huyo aliguswa na tatizo lililowapata na kutoa kiasi hicho cha fedha ili kiweze kuwasaidia waliothirika katika kipindi hicho kigumu.

 



No comments:

Post a Comment