14 January 2013

RC,DC, wapingana Tanga


Na Yusuph Mussa,
Tanga

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Bw. Mrisho Gambo amemtibua Mkuu wa Mkoa wa Tanga Luteni Mstaafu Chiku Gallawa baada ya kuonesha wazi kuwapinga wataalamu waliotoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa huyo kwenda kufanya tathmini kama Mamlaka ya Mji Mdogo Mombo inastahili kuwa Halmashauri kamili ama la.


Bw. Gambo alisema wataalamu hao wana agenda ya siri na hizo ni kampeni wanazofanya na hazitafanikiwa
kwenye hilo, kwani mambo mengi wanayosema kwenye taarifa yao ya tathmini ni ya'kupikwa', huku akisema yupo tayari kuwajibishwa ama kutolewa nje
ya kikao kwa hilo.

Bw. Gambo alipishana 'upepo' na Bi. Gallawa kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambapo walikuwa wanajadili agenda ya Mombo kuwa halmashauri ama la.

"Mwenyekiti (Bi. Gallawa) lazima niseme ili kuitendea haki nafsi yangu, na nipo tayari kuambiwa nifute kauli yangu kwa haya nitakayosema. Mtaalamu hakuwa sahihi katika kuvielezea vigezo vya Mombo kuwa halmashauri au la.

"Kwani vigezo vya mapato vinasema, halmashauri iwe na uwezo wa kujiendesha ni lazima ikusanye asilimia 50, na Halmashauri ya Korogwe Vijijini pamoja na Mji wa Mombo kigezo hicho wamekivuka. Mwenyekiti tunahujumiwa, naomba busara zako zitumike ili
kuondoa hujuma hizo," alisema Bw. Gambo kabla hajazuiwa kuendelea kusema.

"Nimekwambia usirudie kile alichosema mwenzako (Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini Bw.Lucas Mweri),na hapa sisi sio wa mwisho kuna watu watakuja kuangalia kama kweli Mombo inastahili kuwa halmashauri au haistahili," alisema Bi. Gallawa akimuweka sawa Bw. Gambo.

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Bw. Stephen Ngonyani maarufu Profesa Majimarefu, alisema Mombo wana uwezo wa kuendesha halmashauri, na kuomba wapewe nafasi hiyo ili kusogeza maendeleo kwa wananchi.

Akiwasilisha taarifa ya tathmini kwenye kikao hicho, Bw. Yohana Miwa alisema Mombo bado haina uwezo wa kuwa halmashauri, kwani imekosa baadhi ya vigezo ikiwemo mapato ya ndani na idadi ya watu.

Hatimaye mchakato wa Mombo kuwa halmashauri ulipita kwa mbinde, huku Mombo wakitakiwa kuendelea kukamilisha mapungufu yaliyojitokeza kwenye tathmini ya wataalamu.
No comments:

Post a Comment