28 January 2013

Diwani CHADEMA asimamishwa akituhumiwa kuuza chakula cha msaada Kenya


Na Timothy Itembe, Rorya

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Wilaya Rorya kimemsimamisha uongozi kwa muda mwenyekiti wake ambaye pia ni Diwani kata ya Tai, Bw.Goodfrey Masirori kwa tuhuma za kuuza chakula kilichotolewa na serikali kwa ajili ya kugaiwa katika kata ambazo zimekumbwa na baa la njaa wilayani humo.


Akiongea na gazeti hili katibu wa chama Wilaya Rorya Bw. John Oyoo amesema hatua hiyo ilichukuliwa hivi karibuni na chama chake baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wakimtuhumu 
kiongozi huyo kuwa ameshirikiana na viongozi wa vijiji pamoja na  mtendaji wa kata ya Tai kuuza chakula hicho.

Alisema kuwa baada ya kupatikana kwa taarifa hizo chama hakikusita kumchukulia hatua za kinidhamu za
kumsimamisha uongozi kwa muda wa siku 14 kupisha  uchunguzi.

"Hatua ya kumsimamisha uongozi kiongozi huyo 
ilichukuliwa na viongozi wa Chama pamoja na kamati tendaji ambao walihudhuria mkutano ulioitishwa na chama kwa ajili ya kuzungumzia mstakabali wa maendeleo ikiwemo swala la tuhuma za  mwenyekiti huyo

"Baada ya chama kupokea taarifa hizo chama kilichukua hatua ya kumuita mwenyekiti huyo kikaoni kujibu tuhuma ambazo zinamgusa ambapo alijitetea, lakini mazingira yalibainisha kuwa anahusika
na chama kiliamua kumchukulia hatua za kumsimamisha uongozi kwa muda ili kupisha uchunguzi,"alisema.

Bw.Masirori na wenzake ambao ni watendaji wa vijiji vitatu vya kata hiyo akiwemo mtendaji wa kata wanadaiwa kuhusika na kudhulumu wananchi chakula cha msaada magunia 30 ya mahindi ambacho kilitolewa msaada na serikali kwa ajili ya watu wanaokumbwa na njaa wilayani humo ambacho kilitolewa mwaka jana.

Aidha Diwani wa kata ya Mkoma Bw. Razaro kitori alisema kuwa alishuhudia magunia ya mahindi ya
msaada yanashushwa katika kata yake na kuuzwa kwa matajiri wa mji huo bila kumshirikisha, ambapo baada ya kuhoji aliambiwa hana haja ya kujua.

Bw.Kitori ameongeza kuwa mji wake wa Obwere ni kitovu cha biashara wilayani hapo na una wafanya biashara wengi,hivyo kwa hali hiyo alishindwa
kufuatilia baada ya kuona kuwa ni diwani mwenzake ambaye anahusika.

"Chama kama chama kimechukua hatua ya kumsimamisha kazi mwenyekiti kwa uchunguzi ndani ya siku 14 na pia kwa watendaji wa vijiji vitatu vya kata hiyo akiwemo mtendaji wa kata watajadiliwa na kikao cha Halmashauri ya wilaya,"alisema mwenyekiti wa kamati ya uchumi,ujenzi na mazingira, Bw. Thomas Patrick.

Bw. Patrick ambaye ni diwani kata ya Kitembe alisema kuwa tuhuma za mwenyekiti huyo zimekichafua chama, ambapo chama kimechukua hatua ya kumsimamisha uongozi mwenyekiti huyo ili kupisha uchunguzi.


No comments:

Post a Comment