28 January 2013

Vurugu,Rufiji,familia 19 za polisi zaishi kituoni *watu 28 mbaroni


 Na Masau Bwire

WATU 28 wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na uchomaji moto wa nyumba nne za askari wa Jeshi la Polisi na kuteketeza mali zote zilizokuwemo.


Watuhumiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji kwa mashtaka manne yakiwemo ya kuharibu mali na kuchoma nyumba moto katika vurugu zilizotokea mkoani Pwani.

Nyumba hizo zilichomwa moto na wananchi wenye hasira baada ya kupata taarifa kuwa mwananchi mwenzao Hamisi Mpondi, aliyekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuuza bangi amefariki.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani humo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema kuwa kutokana na vurugu hizo nyumba nne za mali za askari polisi zimeteketezwa kwa moto pamoja na mali zote zilizokuwepo.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa asubuhi baada ya wananchi hao kupata taarifa kuwa mwananchi mwenzao amefariki walianza kuvamia nyumba za polisi na kuanza kuzichoma moto na kutoa mali za askari polisi waliokuwa wamepanga katika nyumba za raia.

Kamanda Matei alisema kuwa kutokana na vurugu hizo familia 15 za askari Polisi ambao walikuwa wamepanga katika nyumba za raia mali zao zimetolewa nje na kuchomwa moto.

"Familia 15 za askari Polisi mali zao zimetekea kwa moto baada ya wananchi wenye hasira kuingia na kutoa mali hizo na kisha kuzichoma moto, " alisena kamanda.

Alisema kuwa kutokana na vurugu hizo familia 19 zinaishi katika kituo cha polisi kwa kukosa mahali pa kuishi.

Aidha Kamanda Matei alisema kuwa askari watatu waliokuwa wakienda kuimarisha hali ya usalama wilayani humo walipata ajali maeneo ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam wameruhusiwa baada ya kupata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Alisema kuwa askari mmoja PC Dominick alifariki hata hivyo na askari aliyetambulika kwa jina moja la PC Mathias amelazwa hospitalini hapo kutokana na kujeruhiwa katika maeneo mbali ya mwili.

Hata hivyo Kamanda Mtei aliwaomba wananchi kutii sheria bila kushurutishwa kwani jeshi hilo halitaweza kumvulia mwananchi anayevunja sheria.

"Tunawaomba wananchi wasikubali kurubuniwa kuvunja sheria sisi hatutoweza kuwavimilia kwa uvunjifu wa sheria, " alisema kamanda.

Watu 28 wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Rufiji wakikabiliwa na makosa manne yakiwemo ya kuharibu mali na kuchoma moto ambapo keshoi hiyo itatajwa tena Januari 31, mwaka huu.

Wakati gazeti hili likienda mitamboni, kulikuwa na taarifa kuwa Jeshi la Polisi limetanda katika maeneo mbalimbali wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi mkali ili kuhakikisha kuwa hakuna vurugu zinazojitokeza tena.

No comments:

Post a Comment