28 January 2013

Albino waomba kupewa huduma bure ya DNA



Na Peter Mwenda, Kisarawe

WATU wenye ulemavu wa ngozi (albino) wilayani hapa wameiomba Serikali kutoa bure huduma ya kupima vinasaba (DNA)kuondoa utata katika ndoa zao hasa wanapozaa watoto ambao hawana ulemavu huo.

Wakizungumza katika semina ya siku mbili ya mafunzo ya kujengea uwezo wa viongozi na wanachama wa Chama cha Albino Wilaya Kisarawe, iliofadhiliwa na Taasisi ya Foundation for Civil Service walisema kumekuwa na migogoro mingi kunapotokea kuzaa watoto ambao si albino wakati mume na mke wote ni albino.

"Sisi ambao baba na mama ni albino tunapozaa watoto ambao si albino ndoa zetu zinaingia migogoro mara kwa mara na kusababisha kuachana kwa kukosa elimu hii" alisema Kassim Kibwe.

Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania (CCAT), Ernest Kimaya akifungua mafunzo hayo alisema kumefanyika mpango wa kugawa mafuta laini (Losheni) kwa ajili a kujipaka albino kuanzia ngazi ya wilaya mpaka taifa.

Alisema Serikali imeafiki kutoa matibabu bure kwa walemavu na kuongeza kuwa kutokana na changamoto ya upatikanaji wa dawa katika hospitali nyingi wataiomba Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itoe kadi za Bima ya Afya kwa walemavu ili wapatiwe dawa.

Kimaya pia alitoa wito kwa walemavu nchini kujitokeza kutoa maoni yao nini kiingizwe kwenye katiba mpya kwani mbali a kuundwa kwa sheria mpya ya walemavu haipo kwenye katiba.

Mkufunzi wa mada ya Afya,Dkt.Sobbo Libamba kutoka hospitali Wilaya ya Kisarawe alisema albino wengi huwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa saratani ya ngozi kama hawazingatii kujikinga ngozi yao na jua.

Alisema ili kuwaokoa watoto wadogo albino na athari za jua kali wanatakiwa kuvalishwa nguo ndefu kufunika miili yao,albino wasifanye kazi nje juani,wavae miwani ya jua na kutumia miamvuli.

Naye Daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH),Dkt. Richard Pembe alisema albino anatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa afa ake mara kwa mara na wanapokuwa darasani wakae viti vya mbele kutokana na muono wao hafifu.

Katika semina hiyo iliyowashirikisha albino wa wilaya ya Kisarawe mbali ya kujua changamoto zinazowakabili pia walipewa mafunzo jinsi ya kujiepusha na migogoro ya ndoa kutokana na kuzaliwa watoto ambao si albino.

No comments:

Post a Comment