15 January 2013

Masaburi: Watendaji wanakula fedha za mapatoNa Anneth Kagenda

FEDHA nyingi zinazokusanywa katika taasisi mbalimbali za umma, asilimia tano ya mapato imekuwa ikichukuliwa na watendaji wa kawaida na wale wakubwa wanachukua mara tisa ya fedha hizo.


Mkurugenzi wa Taasisi ya Ununuzi na Ugavi, Dkt. Didas Masaburi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha semina kwa wabunge
wa kamati nne iliyolenga kuwapa elimu ya kujua undani wa
masuala yanayohusu manunuzi ya umma.

Alisema katika taasisi hizo kuna mambo mengi hasa matumizi mabaya ya rasilimali na baadhi ya watendaji wakijihusisha na rushwa jambo linatakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

“Huu ni utafiti uliofanywa duniani kote na kubaini kuwa, asilimia tano za mapato zinazopatikana kwenye Wizara, zinaibwa huku wakuu wa vitengo wakiiba zaidi yani mara tisa,” alisema.

Aliongeza kuwa ni muda mwafaka kwa Serikali kuweka utaratibu katika masuala ya ununuzi hasa kwenye miradi yote ili kudhibiti wizi unaondelea kutokea.

Awali akifunga semina hiyo, Bw. Dastan Kitandula aliwataka wabunge hao kuzingatia yote waliyofundishwa katika semina
hiyo na kuyazingatia ili yaweze kuleta tija siku za usoni.

Dkt. Ramadhani Mlinda ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), alisema
kiwango cha uzingatiaji sheria ya manunuzi mwaka 2010/2011 kilikuwa asilimia 68 mwaka 2011 na mwaka 2012 ilikuwa 74 ambayo ni chini ya malengo.

No comments:

Post a Comment