28 January 2013

Adhabu mbadala jibu la msongamano magerezani



Na Aziz Msuya

MWENYEKITI wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje,Ulinzi na Usalama, Bw. Edward Lowassa amekaririwa akisema kuwa asilimia 90 ya wafungwa walioko magerezani ni vijana


Anasema wamefungwa kutokana na kukutwa na hatia ya kesi ndogo ndogo kama uzururaji,wizi wa kuku na baiskeli ,ulevi,kesi za ndoa na kubambikiziwa kesi na kwamba miongoni mwao ni wale walioshindwa kutoa sh 200,000 kama rushwa ili waweze kupewa dhamana kama ilivyo kwa baadhi ya wafungwa na mahabusu walioko gereza la Segerea.

Bw. Lowassa amesema nchi nzima ina zaidi ya wafungwa 29,000 wakati mahabusu ni 36,552 na kwamba idadi ya mahabusu inazidi ile ya wafungwa kwa asilimia 23 jambo linaonyesha wazi kuwa magereza yamezidiwa uwezo na inaiongezea serikali mzigo wa gharama za kuwahudumia kwa makosa ambayo ni madogo sana lakini kwa wingi huo ni kinyume na haki za binadamu.

Niliwahi kuandika huko nyuma kwamba kuna haja ya Mahakimu na hasa kwenye mahakama za mwanzo ambako ndiko hasa wanakoshughulika na hizi kesi ndogo ndogo kwamba kuna haja ya kuangalia uwezekano wa kutoa adhabu mbadala kwa washtakiwa wanakutwa na hatia ya kesi ndogo ndogo kama hizo ikiwa ni pamoja na vifungo vya nje na kujihusisha na kazi za huduma za jamii.

Kuna adhabu mbadala nyingi sana ambazo kwa namna moja au nyingine kwanza zitapunguza msongamano magerezani,pili zitaipunguzia Serikali gharama za kuwahudumia na pia watasaidia kazi mbalimbali za kijamii kwenye jamii inayowazunguza ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa hukumu zao ambazo zinatokana na makosa waliyoyafanya.

Baadhi ya kazi ambazo wanaweza kuzifanya ni pamoja na kupanda na kuhudumia miti ili kutunza mazingira,kufanya usafi katika maeneo ya kutolea huduma kama hospitalini,mashuleni,kusafisha mitaro ya maji machafu,kufanya usafi kwenye viunga vya miji na majiji,kufyeka nyasi pembezoni mwa barabara halafu gharama ambazo zilikua zilipie utekelezaji wa kazi hizo ziende kuboresha huduma nyingine za kijamii.

Mgawanyo na muda wa kufanya adhabu hizi uwe ni ule ule ulioko kwenye hukumu zao, lakini wazitekeleze wakitokea makwao na sio magerezani tena wafike kwa wakati kwenye maeneo yao ya utekelezaji wa adhabu zao.

Hii itasaidia sana kupunguza msongamano magerezani,kupunguza gharama za kuwahudumia,lakini wakati huo huo kuokoa fedha ambazo zingetumika kufanya kazi hizo.

Ni imani yangu kwamba miongoni mwa wafungwa hawa wapo ambao wana ujuzi na taaluma za fani mbalimbali ni vema wakatumia taaluma zao kwenye kuzalisha mali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa adhabu ambazo wanazitumikia.

Kwa upande wa mahabusu pia kuna haja kwa Jeshi la Polisi kwa maana ya waendesha mashtaka kwa kipindi hiki wakati ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kujipanga ili kuondoa uendeshaji wa kesi mikononi mwa polisi basi ni vema kasi ya upelelezi wa kesi hizi ndogo ndogo ikaongezeka ili hukumu ziweze kutolewa haraka na kwa wakati ili kupunguza msongamano.

Lakini pia madawati ambayo yanapokea malalamiko mbalimbali katika vituo vya polisi ni vema yakajengewa uwezo wa kutoa ushauri pia kwa wateja wao ili wawashauri kwa baadhi ya malalamiko yakamalizwe kifamilia.

Au kwenye mabaraza ya usuluhishi ili kupunguza kila lalamiko kupelekwa mahakamani hii kwa namna moja au nyingine itapunguza idadi ya kesi mahakamani na kutoa fursa kwa kesi zingine kusikilizwa kwa wakati.

Lakini pia ni vema bodi za PAROLE za mikoa zikawezeshwa kufanya kazi zake kwa ufanisi ili kuweza kuangalia uwezekano wa kutoa misamaha kwa wanaostahili, lakini pia kwa kuziangalia hukumu za kesi kama hizi ambazo ni ndogo ndogo zinawezoweza kutafutiwa adhabu mbadala na wakashauri kwa jinsi itakavyoonekana inafaa.

Nionavyo mimi ni muafaka kutumia adhabu hizi mbadala kwa sababu mbali ya faida ya ambazo zitapatikana kama nilivyozitaja lakini itampa fundisho mtuhumiwa kwa sababu inawezekana pia utekelezaji wa adhabu hii ukawa unafanyika hata mtaani kwake.

Na hivyo hali hii itamfanya kujisikia vibaya kwa kua sehemu kubwa ya watu watakaomshuhudia akitekeleza adhabu hii anawafahamu na wanamfahamu pia kwa hiyo kunakuwepo na ile hali ya kupoteza hadhi yake machoni mwa jamii inayomfahamu.

Kila mtu anatamani kulinda hadhi yake machoni mwa jamii ni wachache wasiojali kwa hiyo naamini hatapenda kulirudia kosa alilofanya ambalo kwa kiasi kikubwa limemvunjia hadhi yake kuliko kuitekeleza adhabu hiyo akiwa gerezani ambako haonekani na inawezekana akitoka akahama mji kuficha aibu yake lakini kwa kutekeleza adhabu hii hadharani kutatoa fundisho kwa mfungwa huyo.

Inawezekana tumechelewa kuanza kutumia adhabu mbadala lakini ni vema Vyombo vya Kisheria kwa maana ya Mahakama kujipanga kwa kuangalia njia bora ya namna ya kutekeleza adhabu hizi mbadala.

Ikiwa ni pamoja na kuchota uzoefu kwa nchi ambazo tayari zilishaanza kutumia utaratibu huu ambao kwa kiasi kikubwa utasaidia kupunguza msongamano magerezani kwa kuwa na wafungwa wengi ambao wamehukumiwa kwa kesi ndogo ndogo kama nilivyozitaja.


No comments:

Post a Comment