28 January 2013

"Mbeya msizike walio hai"Na Danny Matiko
HIVI karibuni vyombo vya habari viliripoti tukio la watu watatu kuzikwa kwenye kaburi moja mkoani Mbeya, ambapo wawili miongoni mwa hao walizikwa huku wakiwa hai na afya zao.

Hakika, tukio hilo la kuhuzunisha inasemekana ni ulipizaji kisasi kutokana na imani za kishirikina, ambapo watu hao wawili waliozikwa wakiwa bado hai walishutumiwa na baadhi ya wanakijiji eti walihusika na kifo cha mwanakijiji mwenzao ambaye alifariki kwa maradhi.

Kadhalika, licha ya watu hao waliozikwa hai, na ambao sasa ni marehemu, kudaiwa kutopatiwa fursa ya kujitetea, pia walihukumiwa kinyemela, kwani hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kisheria kilichosikiliza tuhuma dhidi yao na kuzitolea uamuzi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya (RPC), ACP Diwani Athumani, tukio hilo lilitokea Jumapili, Januari 13, 2013, majira ya saa 10 jioni, kwenye kijiji cha Kalungu, Kata ya Ivuna, Tarafa ya Kamsamba, Wilaya ya Momba, Mkoani Mbeya.

Kamanda Diwani alithibitisha kutokea tukio hilo, na pia kuwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya wenzao.

Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika katika unyama huo tayari wanashikiliwa na Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

Akisimulia kuhusu mkasa huo, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Ivuna, Joseph Silwimba Mengwa, alisema alipata taarifa za tukio hilo muda mfupi baada ya kutokea na aliweza kufika haraka kwenye eneo husika na kukuta "watu hao wakiwa wameishazikwa kaburini wakiwa hai."

Inadaiwa kuwa chanzo cha dhahama hiyo ni kifo cha Bw Nongwa Hussein ambaye alikuwa mkazi wa kijiji hicho cha Kalungu, na ambaye aliaga dunia Jumamosi Januari 12, mwaka huu, kufuatiwa kuugua kwa muda mrefu.

Mashuhuda wanaeleza kuwa wakati wa maziko ya marehemu huyo kijijini hapo, ndipo kundi la watu kadhaa, wakiwemo vijana takribani 9, walitoa shutuma kwamba chanzo cha kifo cha marehemu ni kutokana na ushirikina.

Ilidaiwa kuwa shutuma hizo zilipamba moto ambapo kundi la vijana kadhaa lilihamasishana na kuanza kuranda kijijini hapo kuwasaka wale waliodaiwa kuwa ndio wachawi waliomroga marehemu mpaka kusababisha kufikwa na mauti.

Habari zinaeleza kuwa punde kundi la vijana hao lilirejea makaburini likiwa na washutumiwa wao wakiwa hawajitambui kutokana na kupigwa.

Inaelezwa kuwa washutumiwa hao ambao sasa ni marehemu ni Bw Ernest Molela (60) na Bi Mizinala Nachela (50), ambao wote ni wanakijiji hicho cha Kalungu.

Kaka wa marehemu Nongwa, Bw George Hussein, ambaye pia inadaiwa alikuwa ni mmoja wa walengwa wa msako huo alinusurika baada ya wafuatiliaji wake kushindwa kumfikia mara moja.

Taarifa zinaeleza kuwa kutokana na kushindwa kumpata ndugu huyo, hasira za vijana hao zilielekezwa kwenye makazi yake na kuchoma moto nyumba yake.

Kutoka kwenye nyumba hiyo watu hao walitimka mpaka nyumbani kwa Mzee Molela na pia kwa Bibi Mizinala, ambapo waliwakamata kwa pamoja na kuwashushia kipigo hadi makaburini.

Shuhuda wetu ametuambia kwa njia ya simu kuwa mtafaruku uliozuka hapo makaburini uliishia kwa baadhi ya vijana hao kuwavuta washukiwa hao wa ushirikina na kuwatumbukiza kaburini alimokuwa marehemu Nongwa, na kisha kuwafukia sawia wote kwa pamoja.

Hiyo ikiwa na maana kwamba mwili wa marehemu Nongwa ambaye alifariki kifo cha kawaida, pamoja na Mzee Molela na Bibi Mizinala waliokuwa hai, wote kwa pamoja walizikwa katika kaburi moja.

Taarifa zinaeleza kuwa Polisi walipofika kijijini hapo kesho yake walifukuwa kaburi hilo, lakini, hata hivyo, walikuta wale waliozikwa wakiwa hai tayari wamekwishafariki.

Kilichofuata ilikuwa ni kukabidhi miili yao kwa ndugu zao kwa ajili ya kufanyiwa mazishi rasmi, huku mwili wa marehemu Nongwa ukisalia kwenye kaburi lake la awali.

Juhudi hizo za Polisi, ambazo hakika ni za kupongezwa, zilikuwa ni kutaka kuwaokoa ndugu hao wawili waliofukiwa huku wakiwa hai, lakini zilichelewa.

Inafahamika kuwa binadamu aliyefukiwa ardhini akiwa hai hawezi kumudu kuendelea kuwa na fahamu baada ya dakika takribani 3 mpaka 5 hivi, ambapo cha kwanza kuathirika huwa ni ubongo kutokana na kukosa hewa ya oksijeni.

Hakika tukio hilo la kuwazika binadamu wenzetu wakiwa hai ni kitendo cha kinyama na chenye kustahili kulaaniwa vikali na kila mpenda amani, haki na utu.

Kumzika binadamu akiwa hai ni sawa na kuchezea uhai na uzima tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu, ambaye kwa hakika binadamu sote ni sehemu mojawapo ya Uungu wake.

Hulka na asili ya binadamu ni kunusuru uhai wa wengine kwa kadiri inavyowezekana, hata kama ni kwa kupitia katika mazingira magumu.

Juhudi za kuokoa mara nyingi huwa ni ngumu, lakini pia pale inaposhindikana, hulka ya binadamu ni kuokoa miili ya wenzetu waliotangulia na kuizika ipasavyo.

Sasa inakuwa vipi tena wenzetu hao wa kijijini Kalungu kugeuka na kuwazika wanakijiji wenzao huku wakiwa hai?

Juhudi za kutaka kuokoa waliosalia hai mara nyingi huwa ni kubwa kupita kiasi, na ndio maana hata katika tukio la Septemba 11, 2001, ambapo ndege za abiria zilitekwa na magaidi na kulazimishwa kugonga majumba marefu nchini marekani, tuliona jinsi hulka hiyo ya binadamu ya kuokoa wengine ilivyojitokeza kwa haraka.

Katika tukio hilo ambapo jumla ya watu takribani 3,000 walipoteza maisha kutokana na kuangukiwa na majengo hayo, pia waokoaji takribani 350 walifariki wakati wakijaribu kuokoa wale waliokuwa wamenaswa.

Pia, maofisa 60 kutoka vyombo mbalimbali vya usalama wa serikali ya Marekani walifariki wakati wakihangaikia kunusuru maisha ya wananchi.

Kadhalika, kumbukumbu rasmi huonesha kuwa jumla ya miili 295 ya wahanga wa tukio hilo iliokotwa ikiwa "mizima" (ikiwa na viungo vyake vyote), lakini pia jumla ya viungo na mabaki mengine 22,000 ya miili ya binadamu vilipatikana na kuchukuliwa kwenda kufanyiwa mazishi.

Watu kutoka rika mbalimbali walijitokeza na kuitikia wito wa kutoa damu kwa ajili ya majeruhi, ambapo iliripotiwa kuwa jumla ya lita 36,000 za damu zilikusanywa, huku mkasa huo pia ukipelekea watoto 3,050 kupoteza wazazi wao.

Hii yote tunajaribu kuonesha jinsi uhai wa binadamu ulivyo na dhamani kubwa popote duniani, na pia jinsi binadamu wanaosalia hai wanavyotakiwa kujitolea nafsi kunusuru wale wanaojikuta katika hatari na kuelekea kutaka kuangamia.

Hata hao walioshutumiwa kwa ushirikina na kisha kuzikwa wakiwa hai, bado kulikuwa na nafasi ya kuwakamata na kuwafikisha kwenye Kituo cha Polisi ili wafunguliwe mashitaka ya kujihusisha na ushirikina.

Kulikuwa pia na nafasi ya kuviachia vyombo vya dola, ikiwemo mahakama, nafasi ya kushughulikia suala hilo na kulitolea uamuzi ambao, pengine, ungewapatia fundisho ili hatimaye waweze kurejea na kuwa raia wema.

Hata hivyo, kwa kuwa wapigaramli wapo na pia ndio wa kwanza kutoa shutuma dhidi ya wengine, kwa mfano kwamba "fulani ndiye kamuua marehemu", bado jamii isipokuwa makini yaweza kujikuta katika mtafaruku mkubwa wa kuendelea kushikana uchawi.

Ni vyema kukumbuka kuwa wao wenyewe (wapigaramli hao) ni wafanyabiashara, na kwa maana hiyo kauli zao kamwe haziwezi kuwa hakika na sahihi kwa asilimia 100.

Wao, wapigaramli, wanachoangalia ni uwezekano wa kusingizia binadamu wenzao (kuwa ni washirikina) kwa wingi ili kuendeleza utapeli wao. Mbeya kuweni makini.

No comments:

Post a Comment