06 December 2012

Zimamoto yajizatiti kukabiliana na majanga ya moto



Na Peter Mwenda

WATUMIAJI wa barabara wameshauriwa kupisha magari ya Jeshi la Zima Moto na Uokoaji yanapowahi katika matukio ya kuzima moto.


Hayo yalisemwa na Wataalamu wa Tahadhari na Kinga ya Moto, Bw. Lutz Elmers na wenzake kutoka Ujerumani waliokuja kutoa mafunzo ya huduma za zimamoto na uokozi kwenye Chuo cha Zimamoto,Dar es Salaam.

"Madereva wanaoshindwa kupisha magari ya kuzimamoto yawahi kutoa msaada kunaongeza malalamiko kwa wananchi kuwa hawapatiwi huduma kwa wakati" alisema Bw. Elmers.

Akichangia hoja hiyo Mkaguzi Msaidizi ambaye ni Kamanda wa Operesheni Mkoa wa Kinondoni,Bw. Joseph Mwasabeja, alisema kitendo cha Jeshi la Zimamoto kutofika kwa wakati kwenye majanga ya moto husababishwa na madereva wa daladala kukataa kuwapisha wanapokuwa barabarani.

"Baadhi ya madereva daladala wanaposikia king'ora cha zimamoto hawataki kutupisha ili tuwahi katika majanga ya moto hivyo kusababisha tuchelewe," alisema Bw.Mwasabeja.

Katika mafunzo hayo Mkaguzi Msaidizi wa Kitengo cha Usalama kwa Umma, Bw.Elia Kakwembe alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limezijizatiti kukabiliana na majanga ya moto.

Alisema kuanzia sasa wataanza kukagua majengo na vyombo vya usafiri wa nchi kavu na majini kuona kama kumefungwa vifaa vya kuzima moto na wakaokaidi watachukuliwa hatua za kisheria.

Bw. Kakwembe alisema huduma za Zimamoto zinapatikana kwa wananchi kupiga simu bure namba 114 na kueleza eneo ambalo moto umetokea na kuwataka wanatumia namba hiyo kwa mzaha waache tabia hiyo.

Alisema huduma ya Zimamoto ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji hutolewa bure na katika kuongeza ufanisi wanajenga Kituo cha Lugalo ambacho kikikamilika kitakuwa na gari la zimamoto na wagonjwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

1 comment:

  1. KAMA WATANZANIA TUMEJICHUKULIA UHURU KIASI HICHO MPAKA TUOMBWE RIDHAA BKURUHUSU GARI LA ZIMA MOTO LONEWE HURUMA JE IWAPO NI BENKI KUU INAUNGUA,IKULU INAUNGUA TUTAOMBA RUHUSA SASA SIASA IMEINGA JESHINI NI DOSAR KUBWA SANA

    ReplyDelete