10 December 2012
Serikali iwasaidie wajasiliamali kwa kuwapa mafunzo
KUJIAJIRI ni suala linalopewa kipaumbele na mamlaka mbalimbali nchini hata ngazi ya kimataifa.
Kutokana na mabadiliko makubwa katika mifumo ya uchumi, yamechangia watu wengi kukosa ajira ambapo ajira binafsi
ndizo zinazoonekana kushika kasi katika maeneo mengi.
Nchini Tanzania watu wengi wameamua kujiajiri wenyewe wakiwemo wastaafu kwa kufungua vitega uchumi mbalimbali
kama biashara ndogo ndogo ili kujipatia kipato.
Kujiajiri katika biashara ndogo ni jambo jema lakini sisi tunaona kuwa, tatizo kubwa linalowasibu wadau wengi walioangukia katika shughuli hizo ni kukosa mafunzo ya namna ya kuendesha biashara zao na kukuza mitaji yao.
Wafanyabiashara wengi nchini hawabadiliki kwa sababu ya kufanya shughuli zao kwa mazoea bila kuwa na ujuzi wa namna ya kuziendesha hivyo upo umuhimu wa Serikali kubeba jukumu hilo ili kuwawekea msingi mzuri wa maisha.
Wastaafu wengi waliopewa viinua mgongo na kuwekeza kwenye biashara, wanakabiliwa na wakati mgumu kwa sababu ya kutafuna mitaji yao au kuwa na biashara zilizoendelea.
Wanaofanya biashara ya kuuza maandazi na vitumbua hawana mtazamo wa kutunza ziada wanazopata kwa kufungua akaunti, wanachokipata kinakwenda tumboni bila kujua senti 50 inayobaki, ilipaswa kuwekwa akiba ili kuendeleza biashara zao.
Hili ni jambo la hatari sana kwani kundi hili mbali ya kufanya biashara hizi kila siku, litaendelea kubaki maskini bila mafanikio yoyopte kama Serikali haitachukua hatua za makusudi kuhakikisha wanapatiwa mafunzo ya kuendesha na kuendeleza biashara zao.
Serikali na wadau wengine wanapaswa kutambua kuwa kundi hili ni watu wenye vipato vidogo na vya kati ambao hawaweza kulipa maelfu ya pesa kugharamia mafunzo ya uendeshaji biashara.
Umefika wakati wa Serikali kubuni mkakati wa kushirikisha wadau wengine na kuandaa mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji shughuli za ujasiriamali bure
mijini na vijijini bure.
Kwa kufanya hivyo, italeta mwamko kwa wadau hao kujua namna ya kuendesha shughuli zao na kuwapa ubunifu zaidi wa biashara mpya tofauti na sasa.
Kila mtu anafanya biashara kwa kumwiga mwenzake, utakuta kila mahali biashara ni saloon, grosari, maduka ya dawa, chakula na nguo. Je, hivi hizi ndio huduma pekee wanazohitaji wananchi?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment