24 December 2012
Wenyeviti wa vitongoji kulipwa bil. 3.1/-
Na Mwandishi Wetu, Katavi
WAZIRI Mkuu Bw. Mizengo Pinda, amesema fedha zote ambazo wenyeviti wa vitongoji wanaidai Serikali kama posho ya usimamizi katika mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi, zitalipwa karibuni.
Bw. Pinda aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kibaoni, katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kakuni ikiwa ni siku ya 10 ya ziara yake kwenye Wilaya ya Mlele, jimboni kwake Katavi.
Katika mkutano huo, Mkazi wa Kijiji cha Kibaoni, Bw. Wejja Hassan, alitaka kujua kwanini wamelipwa posho ya sh. 10,000, wakati waliacha kazi zao na kutumia muda mwingi kuzunguka
na maofisa wa sensa.
Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema wenyeviti wote waliofanya kazi kwa siku saba na wale ambao maeneo yao yaliongezwa siku
za ziada, watalipwa kwa sababu fedha zimeshapatikana.
“Serikali imeshafanya hesabu zake na kubaini sh. bilioni 3.1 zinahitajika, fedha zimeshapatikana na zitalipwa karibuni,” alisema.
Akijibu swali la Bw. Godwin Mbassa, kuhusu kupanda kwa bei ya mahindi kijijini hapo kutokana na wimbi la viwavi jeshi, Bw. Pinda aliwataka wakazi hao kuanza kuweka akiba ya chakula kwa ajili ya familia zao mara baada ya kuvuna.
“Mnasema bei ya debe moja la mahindi ni sh. 15,000 lakini kwa wenzenu Usevya, wanauziwa sh. 18,000, tatizo la bei halikuja kwa sababu ya viwavijeshi bali ni uzalishaji mdogo msimu uliopita au kutoweka akiba ya chakula baada ya kuvuna.
“Hili ni onyo kwa wakulima, inabidi mkishavuna msiuze chakula chote kwani kuna wakati bei itapanda hivyo jifunzeni kuweka
akiba ya chakula ili muuze zaidi,” alisema.
Alisema kwa wastani, kaya moja inahitaji kuweka magunia 10-15, kama akiba ya chakula mwaka mzima hivyo mtu akivuna magunia 40, atoe akiba ya familia yake na yanayobaki auze.
Bw. Pinda alihitimisha ziara yake Desemba 22 mwaka huu, kwa kufanya kikao cha majumuisho, kuzungumza na viongozi wa
chama na Serikali wa Wilaya za Mlele na Mpanda katika shule
ya Sekondari ya Mizengo Pinda iliyoko Kata ya Kibaoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment