03 December 2012
'Wanaume wakibadilika ukatili wa kijinsia utapungua'
Na Rose Itono
MATUKIO ya unyanyasaji yamekuwa yakishika kasi katika baadhi ya maeneo na kusababisha baadhi ya watu kuamua kukatisha uhai wao kwa kushindwa kuhimili unyanyasaji wanaofanyiwa.
Vitendo hivi vimekuwa vikitokea katika maeneo mbalimbali nchini hali ambayo imekuwa ikisababisha kuendelea kuwepo kwa matukio ya unyanyasaji hasa kwa wanawake na watoto.
Kuna aina nyingi za unyanyasaji wa kijinsia ambazo zimekuwa zikitokea kwa wanawake na wanaume ambapo wengi wamekuwa wakiyaficha manyanyaso hayo kutokana na kuyaonea aibu.
Ukatili wa Kijinsia ni kitendo chochote kinachoweza kumsababishia mtu mwingine madhara kimwili, kiakili, kingono, kisaikolojia, kiutamaduni, maumivu au hata kifo kinachotokea katika familia au jamii.
Ukatili pia humamaanisha vitendo vyenye kusudio la kulazimisha, kutisha au kuogofya mtu na hivyo basi kumshurutisha kufanya jambo kinyume na matakwa yake.
Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo wanaharakati na wadau mbalimbali wamekuwa wakiadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kampeni kabambe ya kimataifa inaongozwa na Kituo Cha Kimataifa cha Wanawake katika uongozi "Women Global Leadership" tokea mwaka 1991 lengo ikiwa ni kuwakomboa watu walioko kwenye mateso hasa wanawake na watoto.
Chimbuko la siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia ni mauaji ya kinyama ya akinadada wa Mirabelle yaliyofanyika nchini Dominika mwaka 1960 na kuanzia Novemba 25 mwaka 1991 Umoja wa Mataifa ulitenga siku hii kama siku ya Kimataifa ya kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake.
Maadhimisho hayo yanafikia kilele Desemba 10 ambayo ni siku ya Kimataifa ya kuadhimisha tamko rasmi la Haki za Binadamu ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili dhidi ya wanawake na haki za binadamu na kutia msisitizo kwamba ukatili kama huu ni uvunjaji wa haki za binadamu.
Kutokana na hali hiyo Jeshi la polisi nchini kwa mara ya kwanza tangu lianzishwe limeungana na wadau mbalimbali kwa kufanya maandamano ya amani kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto.
Jeshi hilo limeamua kufanya hivyo kutokana na ongezeko la vitendo vya ukatili nchini katika maeneo mengi na kusababisha amani kupotea.
Akizungumza na majira katika mahojiano maalumu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela anasema kuwa, kumekuwepo na sababu nyingi ambazo zinapelekea kuwepo kwa unyanyasaji wa kijinsia.
Anasema baadhi ya sababu hizo ni pamoja na biashara haramu ya gongo, matumizi ya madawa ya kulevya na uuzaji wa pombe kali ambazo husababisha ukiukwaji wa haki za binadamu.
Anasema kuwa, vitendo hivyo vimekuwa pia vikitokana na udhaifu wa huduma za kisheria ambapo baadhi ya wanajamii hukosa msaada wa kisheria, kuwepo kwa sheria zilizopitwa na wakati, mitazamo finyu ya waendesha mashitaka mahakamani, makarani, mahakimu na wengine katika usimamizi wa sekta ya sheria.
Anasema kukosekana kwa haya yote kumekuwa kukiwafanya waathiriwa wa ukatili kuendelea kubaki katika maumivu makali maishani.
Anasema kukosekana kwa utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu haki za wanawake kwa dhati kama vile mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake (CEDAW), tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) ni sababu kuu ya kutowajali waathiriwa wa ukatili.
Kenyella anasema kutowaadhibu wanaosababisha ukatili huo ni kuruhusu kuendelea kuwepo miongoni mwa jamii na kuifanya jamii kutoona sababu ya kutoa taarifa pale wanapofanyiwa ukatili.
Anaongeza kuwa, katiba imetoa haki ya usawa baina ya wanawake na wanaume. Hata hivyo sheria nyingi nchini hazifanyiwi marekebisho ili kuweza kuendana na katiba ya nchi.
Anasema kwa upande wa uchumi hali ya ukatili hujitokeza kwa sababu wanawake wengi hawana vyanzo vya vipato na hivyo kuwa tegemezi hali ambayo husababisha kunyang'anywa vyakula na mahitaji mengine ya msingi kama vile mavazi na ada za shule kwa watoto wa kike.
Anasema tabia ya kufanya hivyo ni ukiukwaji wa haki kiuchumi ambapo pia kuna wanawake wamekuwa wakilazimishwa kukabidhi vipato vyao kwa waume zao au rafiki zao wa kiume na ndugu wa marehemu kunyang'anya mali za wajane vimekuwa ni tatizo katika nchi nyingi za Afrika.
Anaongeza kuwa takwimu za kiulimwengu zinaonyesha kuwa, ukatili wa kijinsia hauko kwa wanawake tu bali hata kwa upande wa wanaume ingawa takwimu nyingi zinaonyesha kuwa wanawake ndiyo wahanga wa ukatili kijinsia.
Anasema nchini kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na WHO takwimu zinaonyesha kuwa, maeneo ya majiji kama Dar es salaam asilimia 41 ya wanawake ni waathiriwa wa ukatili wa kijinsia na asilimia 56 ya wale wanaoishi mkoa wa Mbeya hawajawahi kupata ukatili wa Kijinsia GBV kwa wenzi wao.
Anaongeza kuwa, utafiti wa mwezi Mei 2010 uliofanywa na REPOA unaonyesha asilimia 34.8 ya wanawake na asilimia 3 ya wanaume wameshafanyiwa vitendo vya ukatili ambapo mwaka 2007/9 jumla ya kesi 543 kutoka Zanzibar visiwa vya Unguja na Pemba zilitolewa taarifa polisi.
Anasema utafiti uliofanywa na Idara ya Taifa ya Takwimu mwaka 2010 kuhusu hadhi ya wanawake nchini Tanzania ulibaini asilimia 39 ya wanawake wanaafiki kuwa wanaume wana haki ya kupiga wake zao endapo atabishana naye.
Anasema asilimia 37 ya wanawake waliohijiwa wanaafiki kwamba mume ana haki ya kumpiga mkewe kwa sababu ya kuondoka nyumbani bila kumuaga mumewe wakati huo asilimia 40 ya wanawake wanakubali kuwa mume ana haki ya kumpiga mkewe pale anapozembea kuangalia watoto.
Anaongeza kwa upande wa suala la unyumba asilimia 30 ya wanawake wanakubali kuwa mume ana haki ya kumpiga mkewe atakapogoma kufanya tendo la ndoa wakati huo asilimia 53 ya wanawake wanaafiki mume ana weza kumpiga mkewe kwa sababu nyingine yeyote.
Anasema utafiti mwingine uliofanywa Dar es Salaam na TAMWA unabainisha kwamba kati ya wanawake kumi wenye mahusiano ya ndoa na wapenzi wao wanawake tisa wameathiriwa na ukatili wa kijinsia.Pia kati ya wanawake kumi wanawake sita wameathiriwa kimwili.
Anasema pamoja na Jeshi kuanzisha madawati maalumu yuanayoshughulikia unyanyasaji wa kijinsia wapo baadhi ya wanawake ambao bado hawaoni umuhimu wa kuyatumia aidha kwa kuona aibu au kutoyafahamu.
Anasema kutokana na hali hiyo kila mmoja ana wajibu wa kuwa balozi mzuri wa kufikisha ujumbe huu ili kuweza kupunguza tatizo laukatili wa wanawake na watoto ndani ya familia.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa katiba na Sheria Bi.Angellah Kairuki anasema ukatili wa kijinsia unakwamisha maendeleo ya nchi kwa kiasi kikubwa.Hivyo kila mmoja anapaswa kupambana nao kwa kutoa elimu kwa jamii.
Anasema utafiti uliofanyika mwaka 2010 na Idara ya Takwimu ulibaini asilimia 39 ya wanaume wanaamini unyumba ni sehemu ya haki yao.
Anasema vitendo vya ukatili wa kijinsia katika amri kumi za Mungu na kwenye vitabu vya dini zote vinaeleza kuwa wanawake hawapaswi kupigwa bali wanahitaji kulindwa na kuheshimiwa.
Naibu anaongeza kuwa changamoto kubwa iliyopo kufikia malengo ni kutoa elimu ila kila jamii iweze kuelewa haki za binadamu na sera ya taifa ya 2009 ya kuwalinda watoto na wanawake.
Anasema kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Funguka Kemea ukatili dhidi ya wanawake sote tuwajibike' ambayo inasisitiza kuchukua hatua kwa kukemea ukatili dhidi ya wanawake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment