03 December 2012

Tushirikiane kupiga vita ukatili wa kijinsia



Na Rachel Balama

KUMUELIMISHA mwanamke ni njia ya kuitoa jamii inayomzunguka katika umaskini kwani ndiye kiungo cha familia na mzalishaji wa mkuu.

Hii ni sifa mkubwa inayompamba mwananke katika jamii licha ya kutothaminiwa kwa mchango wake kutokana na mila potofu zilizopitwa na wakati.

Mila hizo ni pamoja na kuwa mwanamke ni chombo cha starehe na hawezi kufanya shughuli nyingine ya kumpatia kipato.

Kushikiliwa kwa mila hizo kumesababisha kuwapo kwa ukatili wa wanawake katika jamii nyingi huku wakinyimwa haki zao za msingi.

Kuna aina nyingi za unyanyasaji wa kijinsia na unaweza kutokea kwa wote yaani wanaume na wanawake.

Kwa kawaida unajulikana kama matumizi ya makusudi ya kutumia nguvu na uwezo na kutishia au kwa hali halisi kinyume cha mtu au kikundi au jamii ambapo matokeo yake yanaweza kuleta jeraha au kifo, kuumia kisaikilojia na kutokukua au kudumaa.

Kwa Tanzania unyanyasaji wa kijinsia unafanyika zaidi kwa wanawake ambapo ni pamoja na maneno, sauti, ishara au maonyesho ya sehemu za mwili kwa makusudi kinyume na matakwa ya mtu.

Hakuna mtu anayeruhusiwa kujamiiana na mtu bila ya ridhaa
ya mtu huyo maana hii itakuwa ni ubakaji.

Kumlazimisha mtu kujamiiana nawe kwa kumpa zawadi au kumpa kazi ni unyanyasaji wa kijinsia. Kadhalika, hakuna mtu anayeruhusiwa kushika viungo vya siri vya uzazi, au kumpiga busu mtu bila ya ridhaa yake.

Tendo la ukeketaji ni aina nyingine ya ukatili wa kijinsia. Aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia ni pamoja na kumwita mtu majina, kumlazimisha mtu kuvua nguo mbele za watu au kumlazimisha mtu kujamiiana na mtu mwingine.

Unyanyasaji wa kijinsia ni tendo baya kwa haki za binadamu na unasababisha maumivu kwa wahusika hivyo linahitaji kukemewa kwa nguvu zote.

Tukumbuke kwamba uhusiano wa kimapenzi na watu walio karibu nasi kwa mfano baba, mama, kaka, dada, babu au bibi ni aina nyingine ya unyanyasaji wa jinsia.

Mbali na hayo pia kuna matatizo makubwa yanayowakabili wanawake na ambayo yanahitaji ushauri wa kisheria ni pamoja na suala zima la mirathi na wanandoa wa kiume kushindwa kutunza watoto.

Lakini mkakati uliotumiwa mwaka jana wakati wa siku 16 za kupinga na unyanyasaji wa kijinsia kwa kuhamasisha wanawake kupatiwa ushauri wa kisheria na kisaikolojia umekuwa na mafanikio makubwa.

Wanawake wengi waliweza kutambua umuhimu wa kupata ushauri wa kisheria na pia kujua ni wapi wangekimbilia wanapokutana na matatizo ya unyanyasaji wa aina hiyo.

Pamoja na jitihada za wanaharakati bado Tanzania inaendelea kuwa na visa vya unyanyasaji wa kijinsi kutokana na kuendelea kudumisha mila na desturi zilizopitwa na wakati kunachangia Tanzania kushindwa kufikia usawa wa kijinsia.

Wanaharakati wenyewe wanaweza kupiga kelele lakini linapokuja suala la utamaduni wanasalimu amri na inakuwa ni kikwazo kwao.

Hivyo ni jukumu la kila mwananchi kwa nafasi yake pale alipo kuanza kukemea mila na desturi ambazo zinaonekana kuwa na unyanyasaji wa kijinsia.

Kulingana na ripoti ya shirika la World Economic Forum ya Global Gender Gap 2008, iliyotolewa Novemba 14, 2008, inaonekana nafasi ya Tanzania kushuka katika usawa wa kijinsia ikilinganishwa na mwaka 2006.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba kwa mwaka 2006 ilikuwa nafasi ya -24 duniani na ilishuka hadi nafasi ya 37 mwaka 2007 na nafasi ya 38 mwaka huu.

Lakini pamoja na kushuka huko, nafasi ya taifa hilo la Afrika Mashariki ni nzuri zaidi ikilinganishwa na mataifa mengi ya bara la Afrika.

Tusijivunie kushuka huko na kama tunatakiwa tuendeleze jitihada za kuhakikisha kwamba unyanyasaji huo unatokomezwa.

Usawa wa kijinsia ni muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia mwaka 2015.

Kitu cha msingi ni kuonyesha kujali usawa wa kijinsia kwa lengo la kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO ni kwamba unyanyasaji wa wanawake ni chanzo na matokeo ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.

Wanawake wa vijijini wananyimwa fursa ya kujua masuala ya kupambana na ukatili kutokana na mijadala ya kikanda na kitaifa juu ya masuala ya jinsia kujikita zaidi mijini.

Mara nyingi wahanga wa vitendo hivyo wamekuwa wakipoteza maisha na kupata vilema kwa muda mrefu kutokana na kutokuwa na vituo maalum kwa ajili ya kushughulikia matatizo yao na kuwapatia huduma zote muhimu.

Vitendo hivyo vina madhara makubwa kiafya hivyo ushirikiano kati ya serikali, jamii na wanaharakati unahitajika zaidi ili viweze kuisha.

Pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali na wanaharakati mbalimbali bado tatizo la ukatili linazidi kuongezeka kila kukicha.

Kwa mfano takwimu zinaonesha kuwa asilimia 40-46 ya wanawake nchini wameshafanyiwa ukatili jambo ambalo ni hatari kama hatua hazitachukuliwa mapema.

Ni jukumu la serikali kushirikiana na mashirika pia, jamii kuhakikisha kuwa ukatili nchini unatokomezwa kwa kutimiza mkakati wake wa kuweka vituo vya kutolea taarifa hizo kila mkoa.

Pia viongozi wa kidini na  wa kisiasa kujiunga katika kuelimisha na kutoa ushauri kwa umma kuondokana na vitendo vya kikatili.

Serikali ni lazima kuhakikisha kwamba vitendo vya kikatili vinakomeshwa ili watu waweze kujikita zaidi kwenye masuala ya maendeleo kwa lengo la kufikia malengo husika.

Ni ukweli usiopingika kwamba kama jamii ikishirikiana kwa karibu zaidi upo uwezekano wa kuzuia ukatili wa kijinsia.

No comments:

Post a Comment