05 December 2012
Wamiliki silaha kiholela wapewa siku 30
Na Rose Itono
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imetoa siku 30 kwa watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, kuzisalimisha sehemu husika kuanzia leo kabla msako rasmi haujaanza Januari 5,2013.
Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya ongezeko la vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali.
“Lipo tatizo la kuzagaa na matumizi holela ya silaha isivyo halali, hali hii inachangia ongezeko la matukio ya uhalifu na unyang'anyi nchini kwa kutumia silaha za moto,” alisema.
Aliwataka wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuhakikisha wanazisalimisha kwa Jeshi la Polisi, katika kituo chochote kilichopo karibu yao, kwa Wenyeviti wa vitongoji, vijiji, ofisi za watendaji wa kata, Wakuu wa Wilaya, mikoa, taasisi za kidini ambapo hakuna hatua zitakazochukuliwa kwa watu watakaozirudisha.
Alisema watu ambao watashindwa kusalimisha silaha hizo baada
ya kuda huo kuisha, watachukuliwa hatua za kisheria pamoja na kufikishwa mahakamani kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Aliongeza kuwa, kumbukumbu zilizopo kulingana na operesheni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, zinaonyesha uwepo wa matukio 876
ya uhalifu na unyang'anyi wa kutumia silaha.
Dkt. Nchimbi alisema katika kipindi hicho, silaha 62 ziliibiwa au kunyang'anywa kutoka kwa wamiliki halali ambapo jeshi hilo limeweza kukamata silaha 304 katika matukio ya ujambazi.
“Katika kipindi hicho, matukio ya ujambazi yalisababisha vifo 138 vya raia na askari polisi sita, mali zenye thamani ya sh. bilioni 4.5 ziliibiwa kwa kutumia silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria.
“Zipo silaha ambazo zinamilikiwa kisheria lakini zinatumika kinyume na kuongeza uhalifu nchini hivyo yeyote anayeona anahusika na vitendo hivi ajisalimishe mwenyewe,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment