05 December 2012
Mawakili wavutana kesi ya Lema *Hoja 18 zawasilishwa, umati wafurika kortini
Na Rehema Mohamed
MAWAKILI wa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbress Lema, jana wamewasilisha hoja 18 katika Mahakama
ya Rufaa wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibarila.
Katika hukumu hiyo, Jaji Rwakibarila alitoa hukumu ya kumvua ubunge Bw. Lema ambapo mawakili hao ni Bw. Tundu Lisu na Bw. Method Kimomogoro, waliwasilisha hoja hizo mbele ya majaji watatu ambao ni Salum Massati, Natharia Kimaro na Benard
Luanda waliokuwa wakisikiliza shauri hilo.
Mawakili hao waliiomba Mahakama hiyo ikubaliane na rufaa yao
na kutengue uamuzi wa Mahakama Kuu ya Arusha kutokana na sababu ambazo wataziwasilisha mahakamani hapo.
Kwa nyakati tofauti, mawakili hao walipinga hukumu hiyo wakidai katika hukumu yeke, Jaji Rwakibarila alijielekeza vibaya aliposema mtu yeyote aliyejiandikisha kupiga kura ana haki isiyo na mipaka kupinga matokeo ya uchaguzi.
Akielezea hoja hiyo, Bw. Kimomogoro alisema mtu au mpiga
kura ana haki ya kulalamika kama haki yake ya kupiga kura inapokiukwa.
Naye Bw. Lisu alidai kuwa, wajibu rufaa wakiwa kama wapiga kura hawana haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa ibara ya 26(2) ya katiba.
Alisema sababu za mpiga kura kwenda mahakamani kupinga matokeo kwa madai sheria za uchaguzi zilikiukwa, lazima iendane na haki yake ya kupiga kura akitolea mfano wa kura yake kama isipohesabiwa katika matokeo husika.
Alidai kuwa, mtu aliyepaswa kufungua shauri hilo ni aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Bi. Batilda Buriani, ambapo sheria haiwezi kuruhusu watu wasio na kazi ya maana kwenda kusumbua mahakama wakati muhusika yupo.
Akiunga mkono hoja hiyo, wakili wa Serikali anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Bw. Timon Vitalis, alidai mpiga kura hausiki katika hatua ya kampeni hivyo hapaswi kupinga matokeo ya uchaguzi kwa kasoro zilizojitokeza kwenye kampeni.
“Mpiga kura haki yake ni kusajiriwa na kupiga kura, suala la Bw. Lema kutoa matusi, maneno ya kashfa kwa mgombea wa CCM, je, suala hili linavunja haki gani ya kupiga kura? alihoji Bw. Vitalis.
Akijibu hoja hiyo, wakili wa wajibu rufaa (wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao ndio waliofungua kesi ya msingi), Bw. Arute Mugway, alidai mahakamani ni mahali pa
kudai haki.
Alidai kifungu namba 111(a) cha sheria ya uchaguzi, kinaeleza wazi kuwa mtu aliyepiga kura ana haki ya kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga matokeo ya uchaguzi.
Alisema hoja ya wakili wa Serikali kuwa wapiga kura ni wasikilizaji tu, katika kampeni haina mashiko kwani huenda katika mikutano hiyo kufanya tathmini na kuchagua mgombea wa kumpigia kura
na sio kumsikiliza mtu akiungurumisha matusi.
Hoja nyingine iliyowasilishwa na mawakili wa Bw. Lema ni ile iliyosema Jaji Rwakibarila katika hukumu yake, hakujielekeza katika ushahidi usioacha shaka yoyote.
Walidai katika kesi yoyote ya uchaguzi, ushahidi unaowasilishwa mahakamani unatakiwa uwe na uthibitisho usioacha shaka lakini
Jaji Rwakibarila katika hukumu yake hakuna mahala alipozingatia maneno hayo hivyo uamuzi uliotolewa haulingani na kiwango cha ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.
Akijibu hoja hiyo, Bw. Mugway alikiri Jaji Rwakibarila, kutotumia maneno hayo na kudai alitumia maneno mengine yaliyopitishwa na Bunge na kujiridhisha kuwa, ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo ulikuwa wa kweli usio na shaka yoyote.
Hoja nyingine ya mawakili wa Bw. Lema ni ile iliyosema katika hukumu yeke, Jaji Rwakibarila, alitumia ushahidi wa mdomo bila ushahidi mwingine wa kuunga mkono na kudai kuwa mahakama inaelekeza katika kesi kama hiyo kuwepo na ushahidi wa vielelezo.
Walidai wajibu maombi katika ushahidi wao, walidai kuwa CD za zinazoonesha matukio ya kashfa katika kampeni za Bw. Lema lakini hawakuziwasilisha mahakamani kama kielelezo.
Akijibu hoja hiyo, Bw. Mugway alidai ushahidi wa mashahidi wake uliungwa mkono na mashahidi wote 14 na ulijitosheleza baada ya kusikia na kuona moja kwa moja kampeni na maneno ya kashfa yaliyokuwa yakitolewa na Bw.Lema.
Aliongeza kuwa, CD hizo zilikuwa kwa msimamizi wa uchaguzi hivyo yeye alipaswa kuziwasilisha mahakamani kama ushahidi kwani katika kesi hiyo, yeye alikuwa pande zote mbili.
Wakili wa Serikali Bw. Vitalis pia alizungumzia hoja ya kutolewa kwa matusi katika kampeni na kudai inapaswa kuletwa mahakamani na mtu aliyetukanwa ambaye ni Bi. Buriani.
Alisema kifungu namba 108 cha sheria ya uchaguzi hakitaji matusi kama sababu moja wapo ya kutengua matokeo ya uchaguzi hivyo wabunge wenyewe walipitisha watukanane katika kampenia hata kama Bi. Buriani angefungua shauri hilo yeye mwenyewe.
Akijibu hoja hiyo, Bw. Mugway, alisema moja ya kanuni za uchaguzi zinakataza wanasiasa kutukanana katika kampeni za uchaguzi na kanuni hizo zilisainiwa na vyama vyote vya siasa.
Hoja nyingine waliyoiwasilisha ni ile iliyosema katika hukumu
yeke, Jaji Rwakibarila, hakujielekeza kutumia rejea za kesi ambazo walizitumia kuwasilisha hoja zao kortini ambapo Bw. Mugway alidai jaji alitumia rejea hizo kwa vifungu vya kesi walizozitaja.
Nyingine ni ile waliyosema Jaji Rwakibarila alijielekeza vibaya aliposema kesi za uchaguzi hazikutawaliwa na sheria zinazotumika na nchi za Jumuiya ya Madora (Common Law).
Bw. Kimomogoro alidai mahakama zetu zinawajibika kutumia kanuni na sheria hizo kama zilivyokuwa zikitumika wakati wa uhuru na kutoa mifano mbalimbali ya kesi zilizowahi kuamuliwa kwa kutumia sheria hiyo.
Akijibu hoja hiyo, Bw. Mugway alidai hakuna haja ya kutumiwa sheria hizo kama Tanzania kuna sheria husika zilizotungwa na kudai kifungu cha 1(2) cha sheria ya uchaguzi sura ya 343 kinasema masuala yote ya uchaguzi yatashughulikiwa kwa mujibu
washeria ya uchaguzi.
Hoja nyingine waliyowasilisha inasema mashahidi wa Bw. Lema hawakuwa na ulinganifu kwa sababu wana nyadhifa mbalimbali CHADEMA kwani hata mashahidi wa wajibu rufani
walikuwa wana CCM.
Akijibu hoja hiyo Bw. Mugway alisema mashahidi sita kati ya
14 wa wajibu rufani waliotoa ushahidi wao katika Mahakama
Kuu, hawakuwa wanachama wa CCM.
Baada ya kuwasilishwa hoja za mawakili pande zote, Mahakama hiyo iliahirisha shauri hilo hadi itakapotoa taarifa ya siku ya kutoa hukumu ambapo umati mkubwa ulifurika katika chumba cha mahakama na kumshangilia Bw. Lema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

IWAPO WANAHARAKATI WA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA NA TAMWA WATARUHUSU KES HII YA KIDHALLSHAJI IPINDISHWE UKOMBOZI WA MWANAMKE UTAKUWA NDOTO SHIDA WANAFANYA KAZI KISIASA
ReplyDeleteWATU WASIJIFANYE KUFAHAMU MAMBO AMBAYO UNDANI WAKE HAUJATHIBITISHWA. KULE KUOMBA TAMWA, HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA VIHUSISHWE NA KISHA UNAWEKA KOMENTI KUHUSU WANAWAKE HUO NI UMBEYA HAKUNA JIPYA
ReplyDelete