18 December 2012

Wajadili rasimu ya kuboresha Jiji la Dar


Na Darlin Said

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja
na wadau mbalimbali, wamejadili rasimu ya mpango mpya wa kuboresha Jiji la Dar es Salaam kwa miaka 20 ijayo ambayo italifanya jiji hilo liwe katika mwonekano mpya.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mpango Miji na Vijiji wa Wizara hiyo, Bi. Albina Burra, alisema mpango huo utawapa mwongozo wa kupanga maeneo kutokana na mahitaji yake.

Alisema kutokana na tafiti zilizowahi kufanyika, asilimia 25 tu ya ardhi ndio iliyopangwa katika jiji hilo na asilimia 75 haikupangwa hivyo kusababisha changamoto mbalimbali hususan ujenzi wa viwanda katika makazi ya watu.

“Asilimia 75 ya eneo la jiji hili, halipo katika mpango wa uboreshaji wa mwaka 1979, hali hiyo imechangia kuwepo msongamano wa makazi na shughuli zao kutokaana na udogo wa eneo,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwa kuwa Jiji la Dar es Salaam linakuwa kwa kasi, mpango huo utasaidia kutenga sehemu za makazi, biashara, elimu pamoja na kuboresha sehemu za usafiri wa majini na nchi kavu.

“Utafiti uliopita walitenga asilimia 2 ya eneo kuwa barabara wakati mahitaji ni asilimia 15, hali iliyosababisha kuwepo matatizo ya usafiri jijini Dar es Salaam,” alisema.

Alisema kupitia mpango huo, wanatarajia kupata eneo kubwa zaidi ili kutatua tatizo la barabara  ambalo linawasumbua wakazi wengi, kupanga sehemu za uchumi kama viwanja vya ndege na kuboresha bandari ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya watu.

Bi. Burra alisema mpango huo pia utajadili makazi ya watu na maeneo wanayofanyia shughuli zao ili kuondoa tatizo lililopo
kama kumbi za starehe.


No comments:

Post a Comment