18 December 2012

'Soko huria linachangia kupanda bei ya bidhaa'



Na Kassim Mahege

BAADHI ya wafanyabiashara wa vyakula nchini, wamedai kupanda kwa bei ya vyakula kunatokana na uhuru wa soko huria.


Wafanyabiashara hao wameyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti.

Walisema wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakinunua vyakula vingi kwa bei ya chini na kuvihifadhi na kusubiri
viadimike ili waweze kuviuza kwa bei wanayotaka.

Bw. Idd Selemani ambaye ni mfanyabiashara wa vyakula katika Sokoa la Kariakoo, alisema Serikali haijaamua kumkomboa mkulima kwa kuruhusu soko huria.

“Hali hii imechangia wafanyabiashara wakubwa kuwa na uhuru wa kumkamua mkulima, kimsingi mfumuko wa bei unasababishwa na wafanyabiashara wakubwa, wananunua bidhaa nyingi kwa bei nafuu na kuzificha, zinapoadimika wanazitoa na kuziuza kwa faida kubwa,” alisema Bw. Selemani.

Alisema hivi sasa maharage yamepanda bei kutoka sh.1600 kwa
kilo moha hadi sh. 2000, mafuta ya kula kutoka 13,500 lita tano
hadi sh. 15,000.

Mfanyabiashara mwingine wa bidhaa za chakula Bw. Ismail Juma, alisema bidhaa iliyopanda sana ni unga wa sembe ambapo Oktoba mwaka huu, kilo moja ilikuwa ikiuzwa sh.1000 kwa sasa sh. 1,400.

“Hali hii imechangiwa na uchache wa mahindi, hivi sasa tunanunua mahindi katika soko la Tandale sh. 800 kwa kilo moja wakati miezi michache tulikuwa tunanunua sh. 600,” alisema Bw. Juma.

Alisema mchele nao umepanda kutoka sh. 2,200 hadi 2,500  ambapo wafanyabiashara wenye pesa wananunua bidhaa hiyo na kuhifadhi wakisubiri bei zipande ili wauze kwa faida kubwa.

No comments:

Post a Comment