04 December 2012

'Wafanyakazi muwe makini na vyama vinavyoanzishwa'


Na Mwandishi Wetu

WANACHAMA wa Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini, wamehadharishwa kuwaepuka baadhi ya watu wanaopi sehemu
za kazi na kuwashawishi wajiunge na vyama vipya ambavyo ni
hewa na havina ofisi rasmi.


Tahadhari hiyo imetolewa juzi na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Mahoteli, Majumbani, Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU), Bw. Said Wamba, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa chama hicho Mkoa wa Kinondoni.

Alisema hivi karibuni, wabo baadhi ya watu wanaotumia vibaya sheria ya uanzishaji vyama huru vya wafanyakazi, kutangaza kuanzisha vyama vipya na kuwashawishi wafanyakazi kuhama
katika vyama ambazo wamejiunga navyo muda mrefu.

Aliongeza kuwa, kitendo kinachofanywa na watu hao kinaweza kupoteza umoja na mshikamano wa wafanyakazi nchini hivyo kupunguza nguvu ya kupigania haki na masilahi yao.

“Msingi wa vyama vya wafanyakazi ni umoja na mshikamano miongoni mwao wenyewe kupitia vyama vyao, leo hii kuna watu wanapita na kuwadanganya wafanyakazi wajitoke katika vyama vyenu na kujiunga katika vyama vipya ambavyo havina usajili,
ofisi wala wanachama.

“Wanachama wa CHODAWU tunapaswa kuchukua tahadhari kubwa, tuwaepuke watu hawa, kuanzisha chama cha wafanyakazi mpaka kiweze kusimama chenyewe si jambo la mchezo,” alisema.

Mkutano huo uliitishwa kwa ajili ya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa chama Mkoa wa Kinondoni, ambapo Bw. Wamba aliongeza kuwa, wanachama ndio wenye jukumu la kukijenga chama cha wafanyakazi na kukiimarisha ili kiweze kutimiza wajibu wake.

Alisema hadi sasa, chama hicho kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), wanaendelea kuipigia kelele Serikali ili iweze kuboresha masilahi ya wafanyakazi.

Bw. Wamba alisema, kwa muda mrefu sasa Bodi za kisekta ambazo hufanya kazi ya majadiliano na Serikali kuangalia uboreshaji wa masilahi mbalimbali na mishahara ya wafanyakazi nchini, bado hazijaweza kukaa vikao vyake.

Aliongeza kuwa, hali hiyo inatokana na ukosefu wa fedha ambapo kwa kawaida zinapaswa kukaa kila baada ya miaka mitatu, kupitia upya viwango vya mishahara kwa kila sekta ikiwemo ya binafsi ambayo wafanyakazi wengi ni wanachama wa CHODAWU.

“Hali hii haiwazuii viongozi wa matawi ya CHODAWU kukaa na menejimenti zao kujadili uboreshaji wa masilahi ya wafanyakazi katika sehemu zao za kazi kwa kuanzisha majadiliano ambayo yatawezesha kupatikana mikataba ya hali bora ya kazi.

“CHODAWU ina jukumu kubwa la kuhakikisha jambo hili linafanyika sehemu za kazi kwa kuzingatia sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004,” alisema Bw. Wamba.

Katika uchaguzi huo mdogo, Bw. John Ndomba alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CHODAWU, Mkoa wa Kinondoni baada ya kuwashinda wapinzani wake wawili.

Wapinzani hao ni Beno Tandika na Michael Mpagama nafasi ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Wilfred Mshana ambaye
kwa sasa ni Mwenyekiti wa CHODAWU Taifa.

No comments:

Post a Comment