13 December 2012
Wadau waipinga TANESCO kuongeza bei ya umeme
Na Darlin Said
WADAU mbalimbali wa umeme nchini, wamepinga ombi la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kutaka kupandisha bei ya umeme asilimia 155 kwa miaka mitatu ijayo kuanzia Januari 2013.
Ombi hilo lilikataliwa Dar es Salaam jana katika kikao kilicholenga kujadili marekebisho ya bei za huduma hiyo ambapo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Frateline Kashaga, alisema falsafa ya TANESCO kutaka kupandisha umeme ni ya kisoko
badala ya kumuangalia Mtanzania wa kawaida.
“Lazima tuangalie mazingira ya Mtanzania badala ya soko, kama bei ya umeme itapandishwa wananchi watashindwa kununua huduma hii, asilimia 80 ya Watanzania ni maskini ambao hawawezi kumudi gharama za umeme zinazotumika kwa sasa,” alisema.
Alisema kama Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na
Maji (EWURA), itapitisha ombi hilo, watakaoumia ni wananchi
wa kawaida.
“Nilienda katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda, hali inasikitisha kwani nimefika pale wamewekewa Luku hivyo kusababisha wakati mwingine washindwe, hali hii inachangia wagonjwa kukosa huduma ambayo ni haki yao ya msingi,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa takwimu za EWURA kila mwaka umeme unapanda wakati gesi tayari imegunduliwa hivyo kupunguza gharama ya umeme.
Naye Mhandisi Elizabeth Kingu ambaye ni Makamu Mwenyekiti Baraza la Ushauri la Serikali (GCC), alisema kutokan na hadidu rejea alizopewa (ToR), Mtaalam ushauri amekokotoa bei kwa kutumia vigezo vya uhitaji na upatikanaji huduma ya umeme ambayo si halisi kwa kuzingatia mazingira ya sasa.
Alisema si kila mtu anayetaka umeme anaweza kuupata kwani hauna uhakika pia ni wa kiwango cha chini hivyo ipo haja ya ukokotoaji bei za umeme kuzingatia hali halisi ya uendeshaji, uwezo wa ukusanyaji wa mapato, matumizi na ufanisi wa shirika.
Alisema GCC inaitaka EWURA kabla ya kupandisha gharama za umeme, wajiridhishe na ufanisi wake pamoja na kufanya utafiti kuhusu mwenendo wa kifedha na kiufundi wa TANESCO.
Awali GCC walitaka kujua upandaji bei ya umeme italeta matokeo gani ya kiutendaji kwa kuwa ongezeko la asilimia 40.29 ambalo lilipitishwa Januari 2012 matokeo yake yanatia shaka.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba, hivi sasa TANESCO ina
deni la zaidi ya sh. bilioni 365, hivyo baraza lina mashaka kama wataruhusiwa bado utendaji wake unaweza usiimarike kutokana
na deni hilo kuwa kubwa,” alisema Mhandisi Kingu.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Watumiaji huduma zinazodhibitiwa na EWURA (EWURA CCC), Bw. Said Mohamedi alisema EWURA lazima iweke bayana kutokubaliana na ongezeko hilo ili kumsaidia Mtanzania wa kawaida.
Alisema bei ya sasa ya umeme ni ile ya dharura iliyopitishwa Januari 15 mwaka huu, ambapo hoja inayojengwa ya bei mpya inalinganishwa na ile ya dharura.
Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Bw. Felschami Mramba, alisema shirika liliwasilishamaombi EWURA ili kuongeza bei ya umeme kwa asilimia 155 toka kwenye bei ya wastani sh. 141 kwa uniti.
Alisema lengo la ongezeko hilo ni kukidhi ongezeko la gharama za uendeshaji uliosababishwa na matumizi ya mitambo inayotumia mafuta kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Alisema uamuzi wa kutumia mafuta ilitokana na kuwepo kwa ukame uliyoikumba nchi na kusababisha upungufu wa megawati 350.
Hata hivyo, ingawaje wadau na wananchi walionekana kupinga kupanda kwa bei ya umeme, EWURA walionekana kuunga mkono na kudai ongezeko la bei ya umeme limeisaidia kuimarika mapato
ya TANESCO ambapo deni la shirika hilo linatokana na ukosefu wa fedha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment