13 December 2012

Nyalandu ailipua TANAPA *Wafanyakazi wadaiwa kunyanyasa wawekezaji


Na Grace Ndossa

WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesema baadhi ya wafanyakazi
wa Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), wanashiriki kuihujumu mamlaka hiyo ili kulinda masilahi yao
kwa kupokea rushwa na kuwanyanyasa wawekezaji wazawa.


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu,
alisema tayari Wizara hiyo imewasiliana na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili wafanye uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo na watakaobainika watachukuliwa hatua.

Alisema Serikali haiwezi kuwavumilia au kuwaogopa watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi yao na kuunda mtandao wa kuwanyanyasa wawekezaji wazawa bali wakibainika hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

“Serikali itachukua hatua zaidi kwa Bodi ya Wadhamini kama itabainika imetoa maamuzi yenye athari kwa Taifa yasiyozingatia kutoa kipaumbile kwa wawekezaji wazawa katika tasnia hii ya
utalii nchini,” alisema Bw. Nyalandu.

Aliongeza kuwa, Novemba 23 mwaka huu, Wizara hiyo ilipokea viongozi kutoka Kampuni ya Ahsante Tours iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro ambayo ilifungiwa kuingiza wageni wake katika Hifadhi za Taifa kuanzia Novemba 17 mwaka huu.

Alisema kampuni hiyo ni ya pili kwa kupandisha wageni katika Mlima Kilimanjaro na imeajiri wafanyakazi zaidi ya 600.

Bw. Nyalandu alisema ilidai kutokana na mtikisiko wa uchumi na changamoto zilizosababisha baadhi ya wageni kuahirisha safari za kuja Tanzania mwaka 2011, waliiomba TANAPA iwakopeshe dola za Marekani 70,000.

Deni hilo waliendelea kulilipa kila mwezi na kubakia dola 39 ambazo walishindwa kuzilipa ndani ya miezi miwili mfululizo
baada ya wageni kufuta safari zao kutokana na vurugu za
Jumuiya ya Uamsho Zanzibar.

“Uamuzi wa TANAPA kuifungia kampuni ambayo wao wenyewe waliikopesha, Wizara imeagiza pande hizi mbili zikubalianwe mpango mpya wa malipo usioathiri mwenendo wa uchumi na mapato ya mamlaka,” alisema Bw. Nyalandu.

No comments:

Post a Comment