13 December 2012
Kesi ya Zombe kusikilizwa leo *Serikali yakata rufaa kupinga hukumu ya awali *Yapangiwa Majaji watatu, hoja 11 kuwasilishwa
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA ya Rufaa, Dar es Salaam, leo inatarajiwa kuanza kusikiliza rufaa ya Serikali dhidi ya hukumu iliyompa ushindi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa
Dar es Salaam, ACP Abdallah Zombe pamoja na wenzake.
Rufaa hiyo inatarajiwa kusikilizwa na jopo la Majaji watatu wa mahakama hiyo ambao ni William Mandia, Nathalia Kimaro na Katherine Oriyo.
Mbali na Zombe aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa, washtakiwa wengine walikuwa ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Noel Leonard, Konstebo Jane Andrew, Koplo Nyangerela Moris, Konstebo Emanuel Mabula na Koplo Felix Sedrick.
Wengine walikuwa Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rashid Lema (aliyefariki kabla ya kujitetea), Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.
Bw. Zombe na wenzake walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kukusudia ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, mkoani Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam, waliachiwa huru Agosti 17,2009 na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Wafanyabiashara hao ni Sabinus Chigumbi 'Jongo', Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu (dereva teksi).
Zombe na wenzake walidaiwa kutenda makosa hayo Januari 14 2006, katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam.
Watuhumiwa hao wanarejea tena mahakamani, ikiwa imepita miaka mitatu na miezi mitatu tangu kutolewa hukumu hiyo na Jaji Salum Massati na kuachiwa huru.
Katika hukumu yake, Jaji Massati alisema upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa bila kuacha mashaka.
Alisema mahakama imebaini wauaji halisi hawajafikishwa mahakamani ambapo kutokana na kutokuwepo kwao mahakamani, mashtaka dhidi ya washtakwa hao hayawezi kutengenezeka hivyo akaiagiza Jamhuri iwasake na kuwafikisha mahakamani wauaji halisi.
Hoja za Serikali katika rufaa hiyo namba 254/2009, iliyofunguliwa Oktoba 6, 2009, imebainisha sababu 11 zinazopinga hukumu hiyo na kudai kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washtakiwa wote walikuwa na hatia.
Katika hoja hizo, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) inadai kulikuwa kulikuwa na upungufu katika hukumu hiyo kwa kila mshtakiwa.
DPP anadai Jaji Massati alipotoka na kushindwa kutafsiri sheria pamoja na kanuni mbalimbali zinazohusu mashtaka ya jinai na kwamba alijichanganya sana katika hukumu hiyo.
Alidai kushangazwa na Jaji Massati kushindwa kuwatia hatia washtakiwa wote licha ya kwamba kulikuwa na ushahidi wa
dhahiri na kimazingira wa kutosha kuwatia hatiani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment