28 December 2012

Tunapoihadharisha serikali tuipe na ushauri wa nini cha kufanya



MWAKA 2012, tumepata kuwasikia viongozi wa dini, wasomi, wanaharakati na makundi mengine katika jamii yakiihadharisha Serikali ichukue hatua katika mambo mbalimbali.

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na tofauti kubwa ya kipato miongoni mwa wananchi inayoweza kusababisha kupotea kwa amani tuliyonayo pamoja na tatizo la ajira hasa kwa vijana.

Wapo waliosema upo umuhimu wa Serikali kumaliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi ili kuilinda amani
ambayo inaweza kutoweka kama hazitashughulikiwa.

Wengine wameitaka Serikali kuheshimu misingi ya kidemokrasia kwani bila kufanya hivyo inaweza kusambaratisha amani.

Sisi tunasema kuwa, matatizo tuliyonayo ni mengi lakini bado hayajafikia hatua ya kuvuruga amani na sifa tuliyonayo duniani.

Amani ambayo leo hii tunajaribu kuichezea, ikitoweka kila mmoja wetu atajuta na jitihad za Serikali kukuza uchumi na kuondoa umaskini haziwezi kufanikiwa tena.

Watu wanaotumia kivuli cha dini kutaka kuvuruga amani iliyopo wanapaswa kutambua hakuna dini inayohubiri uvunjifu wa amani.

Upo umuhimu wa viongozi wa dini, wanaharakati na wasomi hamasisha amani na kuishauri Serikali hatua za kuchukua ili kuzikabili changamoto walizonazo wananchi.

Kuihadharisha Serikali katika mambo mbalimbali ni jambo la
msingi lakini tunapoishauri na hatua za kuchukua ili kufanikisha
utekelezwaji wa kile tunachokiamini ni jambo zuri zaidi.

Kwa mfano, tunapozungumzia tatizo la ajira ni vyema tukaishauri Serikali iwezeke zaidi kwenye kilimo na kutoa pembejeo ili vijana wengi washawishike kujishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula, biashara na kubadilisha maisha yao.

Lipo tatizo ambalo limeanza kujitokeza hivi karibuni kwa baadhi
ya vyama vya siasa. Chama tawala kinapotekeleza sera ambayo
wao wanaamini itasaidia kuwakomboa wananchi, chama kingine kinaubuka na kusema hiyo ni sera yao.

Vyama hivyo vinakwenda mbali zaidi na kuipa masharti Serikali juu ya utekelezwaji wa sera husika badala ya kutoa ushauri wao juu ya utekelezaji wake kama tulivyoona kwenye sera ya elimu.

Ukweli ni kwamba, msingi wa demokrasia tuliyonayo ni ule wa vyama husika vya siasa kushirikiana katika mambo mbalimbali
ili kuchochea maendeleo badala ya kuwayumbisha wananchi na
kuwajaza chuki ili kuharibu miundombinu iliyojengwa kwa
gharama kubwa ili kuikomoa Serikali.

Malumbano ya kisiasa ambayo hayana tija kwa wananchi, hayawezi kuboresha maisha yao. Ni muhimu kuishauri Serikali na kuipa mbinu za kutekeleza sera zake kwa manufaa ya Watanzania, kulumbana kwa hoja na kupigania haki kwa njia zinazokubalika.

No comments:

Post a Comment