28 December 2012

'Tunafanyia kazi lalamiko fao la kujitoa'



Na Mwandishi Wetu, Tarime

SERIKALI imewataka wafanyakazi wa sekta ya madini kuwa watulivu wakati ikiendelea kufanyia kazi malalamiko yao juu
ya fao la kujitoa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.


Imesema hivi sasa inaandaa utaratibu maalumu utakaowawezesha wanachama wa mifuko husika kupata mafao yao baada ya kumaliza utumishi wao sehemu za kazi.

Waziri wa Kazi na Ajira, Bi. Gaudensia Kabaka, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mgodi wa dhahabu
wa North Mara, unaomilikiwa na Kampuni ya African Barrick
Gold (ABG), wakati wa ziara yake kwenye mgodi huo uliopo
katika Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Alisema malalamiko yao yamepewa kipaumbele ili kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo ambapo Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), ipo katika jitihada za kuangalia jinsi wanachama walioandikishwa katika pensheni kama wanaweza kuanzishiwa utaratibu wa kuweka na kukopa.

“Serikali itakutana na SSRA pamoja na wadau wa sekta ya madini Januari 7,2013 jijini Dar es Salaam, ili kupata mawazo yao juu ya suala la mafao, wafanyakazi waliopo migodini watawakilishwa na chama chao sehemu za kasi,” alisema.


Aliongeza kuwa, Serikali haina haraka katika suala hilo bali inataka kusikiliza mawazo ya wananchama wote, Watanzania, wabunge na wadau mbalimbali ili kupata maoni ambayo yatatafsiriwa kisheria.

Bi. Kabaka alisema Serikali itawasikiliza Watanzania ili kujua kitu gani wangependa kiwepo katika masuala ya hifadhi ya jamii kwani sheria na sera sio msahafu hivyo inaweza kubadilika kutokana na mahitaji ya wakati husika.

Katika ziara hiyo, Bi. Kabaka alitembelea miradi mbalimbali ya jamii inayofadhiliwa na mgodi huo ambayo ni ujenzi wa shule
mpya na ukarabati mkubwa wa Kituo cha Afya Nyangoto.


No comments:

Post a Comment