05 December 2012

Tunahitaji majibu juu ya wafanyabiashara wanaokwepa kodi



JANA gazeti hili liliandika habari ya uchunguzi juu ya ukwepaji mkubwa wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara  jijini Dar es Salaam, kuingiza mizigo mbalimbali kutoka Zanzibar na nje ya nchi kwa njia za panda na kusababisha Serikali kukosa mapato.

Katika habari hiyo, waandishi walizungumza na baadhi ya watu ambao huendesha maisha yao kwa kubeba mizigo inayoshushwa katika boti katika fukwe za Msasani na Kawe.

Wasiwasi mkubwa walionao wabebaji hao ni aina ya mizigo inayoingizwa na wafanyabiashara husika na kudai kuwa, upo uwezekano mkubwa wa kubebeshwa silaha ambazo zinaweza kuchochea machafuko na kuvuruga amani ya nchi.

Vibarua hao waliongeza kuwa, pamoja na kazi hiyo kuwa ya hatari, ndiyo inayowaingizia kipato cha kuhudumia familia zao na kufanya mambo mengine ya maendeleo mbali ya kulipwa ujira mdogo.

Baadhi ya wavuvi wanaovua samaki katika Bahari ya Hindi nyakati za usiku, nao wameonesha wasiwasi wa kutekwa na wamiliki wa boti zinazotumika kubeba mizigo kama siri hiyo itafichuka na Serikali kuchukua hatua za kuwawinda na kuwakamata.

Lipo tatizo la baadhi ya askari wasio waadilifu ambao wanadaiwa kuwapa ulinzi matajiri wa mizigo hiyo ili wasiweze kukamatwa jambo ambalo uongozi wa Jeshi la Polisi unapaswa kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini askari hao na kuwachukulia
hatua stahiki ili iwe fundisho kwa wengine.

Sisi tunasema kuwa, kutokana na uchunguzi wa habari hiyo Serikali inapaswa kutoa majibu kwa Watanzania juu ya hatua ambazo watazichukua kukomesha vitendo hivyo.

Ukwepaji kodi ni kosa la jinai ambalo hufanywa kwa makusudi
na watu waliodhamiria ili Serikali isiweze kupata kodi ambayo huitumia kuboresha mazingira ya sekta mbalimbali hususan
elimu, afya na miundombinu.

Kama Serikali itashindwa kuchukua hatua za kudhibiti tatizo hilo, upo uwezekano mkubwa wa usalama wa nchi kuwa mashakani kutokana na taarifa zinazodai kuwa, yawezekana miongoni mwa mizigo inayoletwa na wafanyabiashara husika ni silaha.

Ukweli ni kwamba, kama taarifa hizo zina ukweli ndani yake dhana ya Tanzania ni Taifa la amani inaweza kutoweka wakati wowote ikiwa silaha hizo zitatumiwa na waharibu kufanya matukio ya uhalifu na kusababisha vifo hivyo kuongeza umaskini uliopo.

Imani yetu ni kwamba, vyombo vinavyohusika kupambana na uhalifu huu vitawajibika kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzisaka boti zinazobeba mizigo hiyo na wahusika wabanwe
ili wawataje matajiri wasiotaka kulipa kodi.

Vitendo hivi havifanyiki katika fukwe za Msasani na Kawe pekee bali ni pamoja na Bagamoyo ambapo wapo baadhi ya watumishi wa umma ambao hujipatia utajiri wa haraka kwa kuwalinda wahalifu.

No comments:

Post a Comment