04 December 2012

HATARI*Waharifu wadaiwa kupewa ulinzi Bahari ya Hindi *Polisi lawamani, hofu ya kuingizwa silaha yatanda *Wavuvi wahofia usalama wa maisha yao baharini




Na Waandishi Wetu

ULIPAJI kodi si jambo la hiari bali ni lazima ili kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali. Taifa ambalo wananchi wake hawalipi kodi, haliwezi kupiga hatua ya maendeleo.

Mamlaka ya Mapato na Tanzania (TRA), ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kila mwananchi anayestahili kulipa kodi anawajibika kufanya hivyo ambapo Jeshi la Polisi, linapaswa kuzuia mianya
yote ya ukwepaji kodi inayofanywa na watu wasio waadilifu.

Katika kipindi cha miezi zaidi ya sita, gazeti hili lilifanya uchunguzi wa kina usiku na mchana ili kuangalia ukubwa wa tatizo la ukwepaji kodi katika mizigo inayoingizwa jijini Dar es Salaam kwa njia za panya kupitia Bahari ya Hindi, ikitokea visiwani Zanzibar.

Mizigo hiyo hushushwa katika maeneo ya Msasani na Kawe ambapo kazi ya ushushaji shehena ya mizigo katika bodi iznazomilikiwa na watu binafsi hutumia muda usiozidi dakika saba hadi 10.

Uchunguzi wa gazeti

Uchunguzi uliofanywa na Majira, umebaini wapo baadhi ya askari polisi wasio waadilifu ambao hupokea rushwa kutoka kwa matajiri wa mizigo hiyo ili kuwapa ulinzi.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Jeshi la Polisi unapaswa kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini askari wanaofanya vitendo hivyo kinyume na maadili ya kazi zao na kuwachukulia hatua kwani hali hiyo inaweza kusababisha usalama wa nchi kuwa hatarini.

Uingizaji mizigo kwa njia za panya kutoka Zanzibar umekuwa ukifanyika muda mrefu. Boti hizo hupakua mizigo hiyo kuanzia
saa nane usiku hadi 11 alfajiri.

Wakazi waishio jirani na maeneo hayo ambao wamezungumza na gazeti hili, walisema wasiwasi wao ni juu ya mizigo inayoingizwa wakiamini pengine baadhi ya matajiri husafirisha silaha ambazo
wabebaji si rahisi kuzibaini wanapobeba mizigo hiyo kwa ujira mdogo usioendana na kazi wanayoifanya (kujitoa mhanga).

Gazeti hili lilizungumza na mmoja kati ya wabebaji anayeendesha maisha yake kupitia kazi hiyo (jina linahifadhiwa), ambaye alidai uingizwaji mizigo kwa njia za panya umeanza muda mrefu.

“Ngoja niwaeleze ndugu zangu, kazi ya kubeba mizigo haramu inayotoka Zanzibar imeanza kuda mrefu, mimi binafsi naihudumia familia yangu kupitia kazi hii, wapo baadhi ya askari polisi ambao wanatoa ulinzi na kulipwa fedha na matajiri (wahusika wa mizigo).

“Awali baadhi ya boti zilikuwa zikileta mizigo na pale zilipotaka kukamatwa, zililazimika kukimbia majini, sisi tunaamini askari waliokuwa wanataka kuzikamaata walikuwa wageni tofauti na
wale wazoefu ambao wamezoea kuchukua rushwa.

“Mizigo inayoletwa na boti hizi haitokei Zanzibar pekee bali hata katika nchi jirani (jina linahifadhiwa),” alidai mbebaji huyo.

Uchunguzi wa gazeti hili ulikwenda sambamba na uchukuaji picha zinazoelezea uhalisia wa biashara hiyo, zikionesha boti moja iliyokuwa na watu zaidi ya 10, ikishusha mizigo iliyofungwa
katika viroba na kupakiwa katika gari aina ya Hiace (namba
tunazo), ambayo ilikimbia baada ya kuwaona waandishi wetu.

Mvuvi mmoja ambaye alizungumza na gazeti hili (jina tunalo), alisema upo umuhimu mkubwa wa Serikali hasa TRA, kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo kwani kodi inayopotea ni
kubwa kulingana na shehena ya mizigo inayoingizwa kila siku.

Alisema zipo tetesi zinazodai kati ya mizigo inayoingizwa ni pamoja na silaha ambazo hutumiwa na wahalifu katika matukio mbalimbali ya uhalifu na mauaji ili kujipatia utajiri wa haraka.

Aliongeza kuwa, wapo baadhi ya wavuvi ambao hivi sasa wameacha kuvua usiku wa kuanzia saa saba wakihofia usalama wa maisha yao kutokana na taarifa walizopata kuwa kati ya mizigo inayoingizwa na boti hizo ni pamoja na silaha za moto.

“Hadi sasa hakuna mvuvi anayeweza kuhoji na kupata majibu ya mara moja juu ya ukweli wa taarifa hizi, hatujui ni aina gani mizigo inayoingizwa na matajiri kwani hata polisi ambao tunawategemea kwa kuzuia uhalifu, wanatoa ushirikiano kwa wahalifu.

“Huu ni mchezo mchafu ambao uongozi wa Jeshi la Polisi
haupaswi kuuvumilia, hatujui wahusika wa silaha hizi akina
nani na zinakwenda wapi.

“Hivi sasa kumekuwa na matukio ya vurugu mbalimbali nchini hasa zinazochangiwa na imani (dini), hivyo wasiwasi wetu ni kwamba, huenda silaha hizi zikatumika kuchochea mgogoro uliopo,” alisema.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini hakuna mvuvi au mbebaji mizigo aliyeshuhudia uingizwaji silaha katika mizigo hiyo kwa wale waliohojiwa.

Polisi wazungumza

Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema alidai kuwa, yeye binafsi hana taarifa kamili hivyo aliwataka waandishi wafanye mawasiliano na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni.

“Taarifa hizi ndio nazisikia kwenu hivyo tutafanya jitihada za haraka kuhakikisha tunafanya uchunguzi wa kina ili wahusika wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria,” alisema.

Kamanda Charles Kenyela

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema ni kosa kisheria kwa askari kushiriki vitendo vya uhalifu kulingana na kazi yake.

“Siwezi kuthibitisha suala hilo kama lipo au halipo lakini tutafanya uchunguzi na polisi ambao watabainika kujihusisha na vitendo vya aina hii watachukuliwa hatua iwe mfanmo kwa wengine.

“Bahari ya Hindi inalindwa na Jeshi la Polisi Kitengo cha Majini ambao ambao ndio wanapaswa kufanya doria baharini hivyo ni vizuri nao wakapewa nafasi ya kuzungumzia suala hili,” alisema.


Msemaji wa Jeshi la Polisi

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Bi. Advera Senso, alishindwa kuthibitisha madai ya askari kuwapa ulinzi wahalifu wanaokwepa kodi na kusema kuwa, upo umuhimu wa jamii kutoa taarifa za siri kwa uongozi wa jeshi hilo ili wahusika wachukuliwe hatua.

“Mimi sina taarifa na suala hilo ndio kwanza nalisikia, tunawaomba wananchi pindi wanapoona kuna tukio ambalo si zuri, watoe tarifa za siri kwa polisi ili wahusika waweze kukamatwa,” alisema.

Mbunge wa Kawe

Gazeti hili pia lilimtafuta Mbunge wa Kawe, Bi. Halima Mdee, ambaye alikiri kupokea taaarifa za kuingizwa mizigo mbalimbali kutokea Zanzibar kwa njia za panya ili kukwepa kodi hasa nyakati
za usiku.

Alisema baadhi ya askari wasio wadilifu wamekuwa wakilalamikiwa kwa kushindwa kufanya kazi badala yake wanashiriki kutoa ulinzi kwa matajiri wa mizigo inayoshushwa katika boti hizo.

“Malalamiko haya nimeyapata muda mrefu juu ya polisi wetu kuwapa ulinzi wahalifu wanaoingiza bidhaa mbalimbali kwa
njia za panya hivyo kuikosesha Serikali mapato.

“Tatizo jingine ni baadhi ya askari kuwabambikia kesi wananchi, hii ni kero kubwa ambayo uongozi wa Jeshi la Polisi unapaswa kufanya uchunguzi wa haraka,” alisema Bi. Mdee.

Hata hivyo, Bi. Mdee alikwenda mbali zaidi na kuuomba uongizi wa jeshi hilo, ufanye mapinduzi ya kuwabadilisha vituo vya kazi askari waliopangiwa kazi jimboni humo pamoja na kuunda kamati ambayo itafuatilia malalamiko ya wananchi na kuyapatia ufumbuzi.

Diwani Kata ya Kawe

Majira pia lilimtafuta Diwani wa Kata ya Kawe, Bw. Athumani Chipeta, ambaye alidai taarifa za mizigo kuingizwa kwa njia za
panja katika eneo la kata yake ndio kwanza anazisikia hivyo
aliahidi kuzifanyia kazi kwa kuwasiliana na Mkuu wa Kituo
cha Polisi Kawe ili waweze kuchukua hatua.

“Nawashukuru kwa taarifa hizi ingawa ndio kwanza nazisikia hivyo nitakwenda kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Kawe kumweleza ili uchunguzi uanze mara moja kwani wanasababisha Serikali ikose
mapato, kama vitendo hivi vinafanyika katika ufukwe wa Kawe 
basi na ule wa Kunduchi nako si salama,” alisema.

Siku mbili baada ya gazeti hili kuzungumza na Bw. Chipeta, alipiga simu katika chumba cha habari na kudai katika uchunguzi ambao ameufanya, baadhi ya polisi wa Kituo cha Kawe walikiri uwepo
wa tatizo la bidhaa mbalimbali kuingizwa jijini Dar es Salaam
kwa njia za panya katika ufukwe wa Kawe hivyo Serikali
kukosa mapato ambayo yangetokana na kodi.

“Kimsingi nimejaribu kufuatilia ambapo baadhi ya polisi wamekiri kuwepo kwa tatizo la uingizwaji bidhaa linalofanywa na wafanyabiashara hivyo uchunguzi zaidi unafanyika ili
kuwabaini wahusika,” alisema.

TRA wazungumza

Waandishi wetu walifanya jitihada za kuwasiliana na Kamishna wa Upelelezi wa Kodi, Bw. Lusekelo Mwasyeba, ambaye alisema kuwa haitakuwa jambo la busara kulizungumzia suala hilo.

“Si vizuri kuanza kutoa maelezo yanayohusiana na suala hili kwani tayari tunashirikiana na watu flani hivyo tukitoa taarifa za mambo haya tutaharibu upelelezi,” alisema.

2 comments:

  1. SUALA LA KODI NI DONDA NDUGU NCHINI TANZANIA IKIZINGATIWA HAKUNA VITAMBULISHO KWA WANZANIA WANAOJULIKANA NA KUPEWA VITAMBULISHO NI WAFANYAKAZI HAWA HUBANWA WALIPE KODI YA MAPATO [VAT] AMBAYO BADALA KULIPA KWA MWAKANYAVYO KAMA WAFANYAVYO WAFANYABISHARA WAO HULIPA KWA MWEZI HUU NI WIZI KWA WAFANYAKAZI WA NGUVU ZA AKILI ZAO SIDHANI MUNGU ATAENDELEA KURUHUSU DHULUMA HII WATU WENGI HAWALIPIKODI NA WANAOLIPA WANALIPA AU WANAKADIRIWA KODI NDOGO HII INAFANYA KUWE NA PENGO KUBWA LA MAPATO KATI YA MASKINI NA TAJIRI SERIKALI YENYE AKILI ITAFUTE UFUMBUZI

    ReplyDelete
  2. Mbona haingii akilini kwamba bidhaa zinazotoka Zanzibar, zilipiwe ushuru bara!
    Mimi naona tatizo kubwa hapa la kuangalia ni usalama wa nchi (SILAHA) na madawa ya kulevya.
    Pendekezo: Doria za vyombo vya usalama ziimarishwe katika sehemu hizo pamoja na kutumia JWTZ. Askari wanaoshirikishwa doria wawe wanabadilishwa mara kwa mara, kuepusha kuzoeana na maharamia.

    ReplyDelete