05 December 2012
Abood akerwa na ubadhilifu fedha za miradi
Na Ramadhan Libenanga , Morogoro
MBUNGE wa Morogoro Mjini, Bw. Aziz Abood, amesema yupo tayari kukosa ubunge lakini si kuona pesa za miradi zinazotokana
na kodi za wananchi zikitumika vibaya au kutafunwa na watendaji wajanja jimboni humo.
Bw. Abood aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano
wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika katika Viwanja vya Shujaa, Manispaa ya Morogoro Mjini.
Alisema lipo tatizo la ubadhirifu wa fedha katika baadhi ya miradi mbalimbali hivyo kukwamisha maendeleo ya wananchi na kuleta mabadiliko katika manispaa hiyo.
“Manispaa hii ipo katika maandalizi ya kupanda hadhi kuwa jiji hivyo hujuma zinazofanywa na baadhi ya watendaji katika miradi mbalimbali, zinakwamisha kufikia malengo ya manispaa.
“Ipo miradi ya barabara ambazo zimejengwa chini ya kiwango na wakandarasi ambapo watendaji wa halmashauri wenye utalaamu wamekuwa wakinyamaza kimya hivyo ni wazi fedha za Serikali zimekuwa zikitumika vibaya,” alisema Bw. Abood.
Bw. Abood alisema, yeye amechanguliwa na wananchi kusimamia sera na ilani za CCM hivyo yupo tayari kukosa ubunge lakini si
kuwaacha watendaji wabadhirifu wakiendelea kutafuna pesa za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali.
“Nitaendelea kuwaumbua watendaji wote wabadhirifu wa fedha
za miradi hata kama nitakosa ubunge siku zijazo lakini nitakuwa nimesimamia sera na ilani CCM vizuri,” alisema.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro,
Bw. Inocent Karogaries, ambaye pia ni Mbunge wa Morogoro Kusini, alilitaka Baraza la Madiwani wa manispaa hiyo kukaa
chini na kuangalia njia za kumaliza tatizo la wananchi kutakiwa
kulipa bila za maji wakati hawayapati katika maeneo yao.
“Kumekuwa na kero kubwa dhidi ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka mkoani hapa (MORUWASA), kulalamikiwa na wananchi kwa kutoa bili kubwa kwa wateja wakati hawapati huduma ya maji,” alisema Bw. Karogaries.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment