03 December 2012
Tuhuma nzito kwa Jeshi la Polisi Kyela
Na Israel Mwaisaka, Kyela
MKAZI wa Kijiji cha Ipinda, Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya, Bw. Julius Kayombo, amelazimika kuyakimbia makazi yake na kwenda kuomba hifadhi kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani humo Dkt. Hunter Mwakifuna, akihofia usalama wa maisha yake baada ya kutishwa na polisi wa Kituo Kidogo cha Ipinda.
Chanzo cha Bw. Kayombo kuchukua uamuzi huo ni baada ya kutoa kero walizonazo wakazi wa kijiji hicho juu ya manyanyaso ambayo hufanyiwa na polisi wa kituo hicho katika mkutano wa hadhara mbele ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw.
Shamsi Vuai Nahodha.
Mkutano huo ulifanyika hivi karibuni ambapo Bw. Kayombo alidai kuwa, polisi wa kituo hicho huwabambikia kesi wananchi pamoja
na kuwapiga bila sababu za msingi.
Baada ya Bw. Nahodha kusikiliza kero hiyo, aliahidi kulifikisha suala hilo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ili aweze kulipatia ufumbuzi kutokana na uzito wake.
Inadaiwa kuwa, baada ya Bw. Nahodha kuondoka eneo hilo, polisi waliandika barua kwenda kwa Bw. Kayombo (Majira lilifanikiwa kupata nakala yake), iliyomtaka afike afike Kituo cha Polisi haraka
kinyume ya hapo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari, Bw. Kayombo alisema baada ya kuupata wito wa polisi, aliamua kukimbilia kwa Dkt. Mwakifuna, ili kunusuru maisha yake kutokana na hofu aliyonayo juu ya kubambikiwa kesi ya ujambazi.
Kwa upande wake, Dkt. Mwakifuna, alikiri uwepo wa tukio hilo kwa simu ya mkononi na kusisitiza kuwa, ameamua kumpokea
Bw. Kayombo wakati akitafuta suluhisho la tatizo hilo.
“Baada ya kupata malalamiko haya, nilimtafuta Mkuu wa Polisi wilayani hapa ili kuona namna ya kutatua mgogoro huo ambao unahitaji kupata ufumbuzi wa haraka,” alisema.
Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bw. John Komba, alisema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imepokea malalamiko hayo ambapo tangu jana ilikuwa ikilishughulikia tatizo hilo.
Alisema kitendo cha polisi kutumia madaraka yao kumwadhibu
mtu anayetoa taarifa kwa kiongozi wa juu serikalini ni utovu wa nidhamu na vinachangia kulishushia heshima jeshi hilo pamoja
na Serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment