03 December 2012
Tanzania yakibana kituo cha CNN
Na Grace Ndossa
SERIKALI ya Tanzania imekitaka Kituo cha Television cha CNN, kukanusha habari za upotoshaji ilizozitoa kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, katika Ziwa Nyasa.
Habari hiyo ilirushwa na kituo hicho nchini Marekani kuanzia Novemba 24-26 mwaka huu, ikionesha mpaka wa Tanzania upo ukingoni mwa ziwa hilo badala katikati.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Bw. Assah Mwambene, alisema kituo hicho kilirusha vipindi vyenye upotoshaji na kutumia ramani
isiyo sahihi.
Alisema kutokana na upotoshaji huo, Serikali imechukua hatua ya kuuandikia barua uongozi wa CNN ili ukanushe habari hiyo mara moja.
Aliongeza kuwa, mgogoro bado upo na mazungumzo yanaendelea ambapo hivi sasa umefikishwa katika Baraza la Marais 10 wastaafu wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ili kuusuruhisha.
Bw. Mwambene alisema kama mgogoro huo ukishindikana kupatiwa ufumbuzi katika baraza hilo, utapelekwa mahakamani.
Wakati huo huo, Bw. Mwambene alisema Maadhimisho ya Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Bara, yatakayofanyika Desemba 9 mwaka huu katika Viwanja vya Uhuru, Dar es Salaam.
Alisema maadhimisho hayo yatakwenda sambamba na sherehe za mafanikio makubwa ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya nne.
Aliongeza kuwa, mafanikio hayo ni pamoja na Serikali kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya barabara ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema, “Uwajibikaji, uadilifu na uzalendo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa letu”.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment