19 December 2012
TMA yazindua njia mpya za kutoa taarifa
Jane Hamalosi na Neema kalaliche
MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imezindua njia mpya ya kutoa taarifa zake za hali ya hewa na tahadhali kwa wananchi kupitia mtandao wa Vodacom.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi, aliyasema hayo
Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
“Tanzania ni kubwa na hali ya hewa katika maeneo mengi inatofautiana, wakati mwingine njia zinazotumika kutoa taarifa haziwafii watu wote kwa wakati hivyo njia ya simu za mkononi
ni bora zaidi, asilimia kubwa ya Watanzania wanamiliki simu,” alisema Dkt. Kijazi.
Aliongeza kuwa, taarifa hizo zitapatikana kwa Kiswahili na Kiingereza zikionesha hali ya hewa ya mawingu, upepo, unyevunyevu na hali ya bahari kwa mikoa yote nchini.
Alisema mamlaka hiyo inajitaidi kutumia fursa za teknolojia zilizopo ili kuhakikisha Watanzania wanapewa taarifa za hali
ya hewa kila mara wanapozihitaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Vodacom, Bw. Kelvin Twissa, alisema huduma hiyo itawahusisha wateja wa mtandao wa Vodacom.
“Mteja wa Vodacom atatakiwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno katika namba 15588 na itagharimu sh. 100 kwa kila taarifa,” alisema Bw. Twissa.
Alitoa wito kwa Watanzania kutumia fursa hiyo ili kupata taarifa za hali ya hewa, kujenga utamaduni wa kutafuta na kupata taarifa hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment