19 December 2012

LHRC chalaani mauaji ya polisi




Na Agnes Mwaijega

KITUO cha Sheria na Haki Binadamu (LHRC), kimetoa tamko la kulaani mauji ya polisi wawili yaliyotokea katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Helen Kijo-Bisimba, alisema
mauaji hayo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Aliongeza kuwa, Serikali inapaswa kuchukua hatua ili kuhakikisha vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi katika jamii vinakoma.

“Tunatoa pole kwa uongozi wa Jeshi la Polisi ambalo limepoteza watendaji wake na tunalaani kwa nguvu zote mauaji ya kikatili, Serikali ichukue hatua dhidi ya wote waliohusika,” alisema.

Alisema mauaji ya raia na polisi ambayo yamekuwa yakitokea
mara kwa mara nchini ni hatari kubwa kwa Taifa na yanachangia  kukuza uhasama kati ya polisi na raia.

“Naiomba jamii iache utamaduni wa kujichukulia sheria mkononi, hii ni hatari kwa mustakabali wa amani na utulivu katika nchi,” alisema Dkt. Bisimba.

Aliongeza kuwa, malalamiko yao dhidi ya Serikali kutokana na mauaji yanayotokea nchini, tayari wameyapeleka katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu (ICC), ambayo yameanza kufanyiwa kazi.

Septemba 28 mwaka huu, LHRC iliishtaki Serikali kutokana katika mahakama hiyo kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya mauji ya watu mbalimbali wasio na hatia.

No comments:

Post a Comment