04 December 2012

TCRA kujadili changamoto za kuhamia mfumo mpya digitali



Na Darlin Said

MAMALAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA), inatarajia kufanya mkutano 12 wa utangazaji ambao utatanguliwa na warsha ambayo itajadili changamoto zinazotokana na kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda dijitali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Bi. Rehema
Makuburi, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kauli mbiu ya mkutano huo ambao utafunguliwa na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal inasema; “Changamoto na faida kuelekea mfumo wa utangazaji wa Digitali”.

Aliongeza kuwa, mkutano huo utafungwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara.

Bi. Makuburi alisema zaidi ya watu 100 watahudhuria mkutano huo kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo wawakilishi kutoka nchi za Italia, Uingereza na Kenya ambao wataonyesha vifaa vya utangazaji.

“Hadi sasa changamoto tuliyoigundua ni jamii kubwa kutoelewa dhana ya kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda dijitali, watu wanafikiri katika mfumo mpya, televisheni na dish zao haziwezi kutumika tena jambo ambalo si kweli,” alisema.

Aliviomba vyombo vya habari na wadau wengine kutoa elimu zaidi kwa jamii ili iweze kuelewa na kuwa tayari kutumia mfumo mpya.

Alisema ili kulinda maadili utangazaji,  TCRA imejipanga vizuri kuhakikisha yanazingatiwa pamoja na kutoa mafunzo kwa watangazaji nchini.

No comments:

Post a Comment