18 December 2012

TCIB waitaka NEC ibadilishe matokeo ya udiwani



Na Mariam Mziwanda

KITUO cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB), kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ibatilishe matokeo ya chaguzi za madiwani zilizofanyika hivi karibuni kutokana na matatizo
yaliyojitokeza katika chaguzi hizo.


Mkurugenzi wa kituo hicho, Bw. Deus Kibamba, alisema miongoni mwa matokeo ambayo ni batili kwa mujibu wa uchunguzi wa kituo hicho ni kiti cha udiwani eneo la Magomeni, Wilaaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani.

“Kutokana na ridhaa NEC kwa TCIB kuwa mwangalizi wa chaguzi uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 29 Tanzania bara, sisi tumekabidhi taraifa ya uangalizi kwa tume.

“Pia tumetoa mapendekezo kwa ajili ya uchaguzi wa siku zijazo kutokana na kasoro tulizoziona, kituo hicho kimebaini mwitikio
duni wa wananchi kupiga kura unaodumaza dhana nzima ya demokrasia ya uwakilishi kupitia uchaguzi,” alisema.

Alisema katika chaguzi hizo kulikuwa na maudhulio hafifu ya wapiga kura katika Kata ya Mtibwa, Mvomero, Kilema Kusini na Likokona wakati Kata ya Magomeni wilayani Bagamoyo, ilikuwa
na wapiga kura asilimia 14 ambao ndio waliomchagua diwani.

“Tunaitaka NEC ifute matokeo ya kata hii, pia lipo tatizo la wananchi wengi kunyimwa fursa ya kupiga kura na kubainika
taarifa tofauti za takwimu zilizomo katika daftari la kudumu la wapiga kura,” alisema.

Bw Kibamba aliongeza kuwa, msimamo wa kituo hicho juu ya mapendekezo yake kwa NEC ni kuwa na ofisi katika kila Wilaya ambapo mchakato wa kuhakiki wa wapiga kura uwe endelevu na kutengewa bajeti mapema kuanzia Julai 2013.

“Imani ya wadau wa uchaguzi wakiwemo vyama vya siasa na wapiga kura ni kutokuwa na imani na NEC ambayo viongozi
wake wakuu wanachaguliwa na Rais ambaye ndiye Mwenyekiti
wa chama tawala CCM,” alisema.

Pia kituo hicho kimelalamikia uvunjifu wa sheria, kanuni, miongozo, uwepo wa fujo, vitisho na matumizi ya silaha katika chaguzi za madiwani hivyo kusababisha uvunjifu wa amani.

Kwa upande wake, Ofisa Utawala wa kituo hicho, Bi. Debora Mushi, alizitaka taasisi za kiraia nchini kuamka na kueneza elimu juu ya umuhimu wa wanawake kuwania uongozi kwani wengi wao hawajui haki zao hivyo kushindwa kutumia fursa walizonazo.

No comments:

Post a Comment