10 December 2012
Shahidi amlipua mshtakiwa anayedaiwa kumtesa mtoto
Na Rashid Mkwinda, Mbeya
SHAHIDI wa mwisho katika wa kesi ya kumtesa mtoto Ainessy Gasto (3) inayomkabili Bahati Mkandara ambaye ni shangazi wa mtoto huyo, Sajenti Prudensiana, jana alitoa ushahidi wake katika
ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mbeya.
Akiongozwa kutoa ushahidi huo na Mwendesha Mashtaka wa mahakama hiyo Bw. Achilesi Mulisa, mbele ya Hakimu Mkazi, Gilbert Ndeuruo, alisema mshtakiwa alikuwa akimpiga, kumgongesha kichwa ukutani na kumsababishia majeraha.
Alisema alipokutana na mtoto huyo kwa mara ya kwanza,
alikuwa na majeraha makubwa kichwani na mkono wa
kushoto ambao baadaye ulilazimikwa kukatwa.
Aliongeza kuwa, mtoto huyo alidai shangazi yake alikuwa akimpiga hadi kumvunja mkono huo na kusababisha ashindwe kufungua mlango hivyo alilazimika kujisaidia ndani.
Shahidi mwingine ambaye ni Daktari wa Magonjwa ya Akili
katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Dkt. Trioala Nyenza, alisema mshtakiwa alifikishwa hospitalini hapo wodi ya wagonjwa wa akili ili aangaliwe kama alikuwa na matatizo.
Alisema alimfanyia uchunguzi mara tatu kwa nyakati tofauti na kubaini mshitakiwa hakuwa na matatizo yoyote ya akili ambapo vitendo hivyo alivifanya akiwa na akili zake timamu.
“Nilikaa naye muda mrefu na kumchunguza akili yake, mara tulikaa Novemba Novemba 14, kikakaa naye tena Novemba 28 na mara ya mwisho ilikuwa Desemba 4 mwaka huu, nimebaini hana matatizo yoyote ya akili na alifanya vitendo hivi kwa kudhamiria,” alisema.
Kwa upande wake, Mwendesha Mashataka, Bw. Mulisa, alisema upande wa mashtaka umemaliza kutoa ushahidi wake hivyo Mahakama inasubiriwa kwa hatua nyingine.
Hakimu Ndeuruo alimpa nafasi mshtakiwa ili aweze kujitetea na kudai anawasiliana na mumewe ambaye ameahidi kumleta wakili atakayemtetea baada ya wiki moja. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 20 mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment