10 December 2012

Daktari, Muuguzi kortini kwa rushwa *Wote ni wa kitengo cha MOI Muhimbili



Na Rehema Mohamed

DAKTARI na Muuguzi mmoja wa Kitengo cha Mifupa (MOI), katika Hospitari ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na shtaka la kuomba na kupokea rushwa ya sh. milioni 1.5.


Washtakiwa hao ni Bi. Deodata Maliko (30), ambaye ni daktari, mkazi wa Upanga na Muuguzi, Bw. Erick Kimwomwe (38),
mkazi wa Ubungo Kibangu.

Mbele ya Hakimu Hellen Liwa, wakili wa Serikali kutoka Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Allen Kassamara, alidai washtakiwa hao walitenda makosa hayo
Novemba mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Akisoma shtaka la kwanza, Bw. Kassamara alidai Novemba 27 mwaka huu, katika kitengo hicho, washtakiwa hao waliomba
rushwa ya sh. milioni 1.5, kutoka kwa Bw. Sandford Muhina.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao waliomba
fedha hizo ili waweze kumfanyia wa haraka Bw. Fanuel Gideon, ambaye ni upasuaji mgonjwa wa Bw. Muhina, ambaye alilazwa katika wodi namba 18, Sewahaji.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa Novemba 29 mwaka huu, washtakiwa hao wakiwa watumishi wa umma katika hospitali hiyo, walijipatia sh. milioni moja kutoka kwa Bw. Muhina kama kishawishi cha kumfanyia upasuaji wa haraka mgonjwa wake wakati wakijua upasuaji huo upo ndani ya majukumu yao.

Washtakiwa hao walikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Wakili Liwa alidai washtakiwa hao watapewa dhamana kama watakuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambulika
na Serikali ambao watasaini bondi ya sh. milioni 1.5 kila mmoja.

Pia washtakiwa haowametakiwa kutosafiri nje ya Mkoa wa
Dar es Salaam bila ya kibali cha Mahakama.

Bi. Maliko alifanikiwa kutimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana wakati Bw. Kimwomwe akirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti hayo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 20 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment