04 December 2012

Rufaa ya Lema kuanza kusikilizwa leo


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Rufaa jijini Dar es Salaam, leo inatarajiwa
kuanza kusikiliza rufaa ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha
Mjini, Bw. Godbless Lema (CHADEMA).

Rufaa hiyo inatarajiwa kusikilizwa na jopo la Majaji watatu ambao ni Salum Massati, Natharia Kimaro na Bernard Luanda ambapo shauri hilo litaanza kusikilizwa saa tatu asubuhi.

Bw. Lema alikata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa Aprili 5
mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, chini ya Jaji Gabriel Rwakibarila, ambaye alikubaliana na hoja za
walalamikaji hivyo kumvua ubunge.

Novemba 8 mwaka huu, Mahakama hiyo ilimtaka Bw. Lema awasilishe rufaa yake upya baada ya kuifanyia marekebisho na kukataa ombi la wajibu shauri ambao ni wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Awali mahakama hiyo ilikubali kuwa, rufaa ya Bw. Lema ilikuwa
na kasoro lakini ilimtaka aifanyie marekebisho na kuiwasilisha tena ili usikilizwaji wake uweze kuanza.

Hata hivyo, katika uamuzi wake kwenye pingamizi hilo, Mahakama hiyo ilidai kasoro hizo haziwezi kuifanya rufaaa hiyo ifutwe kwani tatizo lililojitokeza halikufanywa na Bw. Lema bali limefanywa na watendaji wa mahakama.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama hiyo ilimpatia Bw. Lema siku 14 kuanzia Novemba 8 mwaka huu, awe amewasilisha upya rufaa yake ambayo ameifanyia marekebisho.

Aprili 5 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitoa hukumu ya kumvua ubunge Bw. Lema, kutokana na kesi ambayo ilifunguliwa na wanachama watatu wa CCM.

Wanachama hao ni Bw. Mussa Mkanga, Bi. Happy Kivuyo na Bi. Agnes Mollel, wakipinga ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

Bw. Lema alikata rufaa mahakamani kupitia kwa wakili wake Bw. Method Kimomogoro, kupinga hukumu ya Mahakama Kuu na kutoa hoja 18.

No comments:

Post a Comment