04 December 2012
NEMC yatoa tahadhari kwa wananchi, Viwanda
Na Jovin Mihambi, Simiyu
BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limewahadharisha wamiliki wa viwanda na baadhi wananchi kuacha kujenga majengo kando ya ziwa, bahari na mito kuepuka usumbufu wanoweza kuupata kama hawatafuata taratibu.
Ofisa kutoka NEMC, jijini Mwanza, Bw. Boniphace Guni, aliyasema hayo juzi katika mahojiano na gazeti hili.
Alisema lipo tatizo la baadhi ya wamiliki wa viwanda na wananchi kujenga majengo kando ya mito, bahari na ziwa bila kuacha mita 60 kutoka ndani ya eneo husika,
Alisema sheria za hifadhi mazingira kifungu nambari 191 ya mwaka 2004, inahimiza wadau wa mazingira kuheshimu sheria hiyo ambapo viwanja na nyumba zilizojengwa kabla ya kutungwa sheria hiyo bado hawajafanya marekebisho ambayo yatalinda mazingira.
“Ofisi yetu itaendelea kutembelea maeneo haya na kutoa ushauri ili wahusika waweze kufanyiwa uhakiki wa athari zinazotokana na shughuli zinazofanywa katika sehemu walizopo,” alisema.
Aliongeza kuwa, tatizo hilo pia husababishwa na watendaji wakuu kuanzia mamlaka za vijiji hadi majiji kutozingatia sheria za mazingira hivyo kutoa vibali vya ujenzi wa viwanda na nyumba kando ya mito, ziwa na bahari bila kuzingatia sheria.
Bw. Guni alisema mbali na ujenzi usiozingatia hifadhi mazingira, wapo baadhi ya viongozi ambao wamepewa mamlaka ya kusimamia sheria ndogo ndogo za vijini na majiji kuruhusu shughuli za kilimo zifanyike katika maeneo hayo.
“Katika barabara ya Kenyatta na Nera, viwanda vilivyojengwa kando ya Ziwa Victoria ni hatari kwa mazingira ya ziwa na
viumbe vinavyoishi humo,” alisema.
Alisema kutokana na shughuli za kilimo zinazoendelea katika maeneo hayo, halmashauri ya jiji hilo kupitia kitengo chake cha hifadhi ya mazingira, haina budi kusimamisha kilimo hicho.
Aliongeza kuwa, dawa za kuua wadudu katika kilimo cha mboga mboga zinasambaa katika Ziwa Victoria wakati wa mvua hivyo kuchafua mazingira na kuhatarisha uhai wa viumbe wa majini hususan samaki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment