13 December 2012
Raia wa Rwanda waingia Tanzania kuomba hifadhi
Na Theonestina Juma, Kagera
ZAIDI ya raia 40 kutoka nchini Rwanda wengi wao wakiwa wanawake, wameingia nchini katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera ili kuomba hifadhi.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Constantine Kanyasu, amethibitisha kuingia kwa watu hao tangu Desemba 6 mwaka huu, baada ya kuvuka Mto Kagera kwa mtumbwi katika eneo la Mafiga Matatu, lililopo mpakani mwa Tanzania na Rwanda.
Alisema watu hao wamekimbilia nchini ili kunusuru maisha yao kutokana na kundi la watu kuvamia nyumba zao usiku, kuwagongea milango, kupora mali, kubaka wanwake, kuwakamata waume zao na kuwapeleka mahali pasipojulikana.
“Baada ya kuwabana ili kujua kwanini wanakimbilia Tanzania, hayo ndio waliyotueleza, wao wenyewe wanwatafuta waume zao ambao hawapatikani hata katika simu za mkononi,” alisema Bw. Kanyasu.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo alifanya mawasiliano na Meya wa Wilaya ya Kirehe, nchini humo ambaye alidai katika maeneo wanayotoka watu hao hakuna hakuna vita, wala
wachafuko yoyote kama inavyodaiwa na raia hao.
Alisema Meya huyo alidai watu hao wanakimbia matatizo ya kijamii hivyo wanaamua kukimbilia Tanzania ili kutafuta ajira.
Bw. Kanyasu alisema, baadhi ya raia hao kubaini uongozi wa Wilaya unafanya mawasiliano na Serikali ya Rwanda waliondoka
na kwenda nchi jirani ya Burundi kwa jamaa zao.
Alisema hadi jana, raia 19 wa nchi hiyo ndio waliobaki lakini kuna wengine watano ambao wameingia wilayani humo wakitokea nchini humo hivyo kufikia 24 miongoni mwao wanaume sita.
“Watu hawa wametokea Wilaya ya Kiteranyi na Kirehe nchini humo na wamewekwa katika Kijiji cha Kasange, hadi sasa tayari nimewasiliana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa ili iweze kutupa utaratibu na namna ya kuwahifadhi,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment