13 December 2012

Pinda kuanza ziara ya siku 13 Katavi



Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Bw. Mizengo Pinda, leo anaanza ziara ya siku
13 katika Jimbo la Katavi, Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi kwa kutembelea kata zote za wilaya hiyo, kufanya mikutano ya
hadhara na kukagua baadhi ya miradi ya maendeleo.


Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, imesema Bw. Pinda ataanza ziara yake katika Kata ya Inyonga, Ilunde, Ilela, Nsenkwa, Utende na Uruwira.

Baada ya hapo atakwenda katika Kata za Ugalla, Litakumba, Nsimbo, Kapalala, Mtapenda, Kasokola, Magamba, Itenka, Machimboni, Sitalike, Kibaoni, Kasansa na Mamba.

Bw. Pinda pia atatembelea Kata za Majimoto, Mwamapuli,
Usevya, Mbede, Ikuba na kurejea tena Kibaoni ambako
 atakuwa na mapumziko ya sikukuu ya Krismasi.

Baadhi ya shughuli kubwa ambazo Bw. Pinda amepangiwa kuzifanya katika ziara hiyo ni kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara ambayo itafanyika kila kata.

Pia atafungua mabweni na kukagua ujenzi wa nyumba za walimu katika Sekondari ya Ilela, kuweka jiwe la msingi katika Zahanati ya Nsenkwa, kukagua kituo cha afya na kuzindua mradi wa madawati kwa shule za tarafa ya Inyonga.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Bw. Pinda pia atakagua miradi ya kilimo Mwamapuli na kuzindua mradi wa umeme jua kwenye
Shule ya Sekondari Usevya.

Mkoa mpya wa Katavi ambao ulizinduliwa rasmi Novemba 25 mwaka huu na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal,
una Wilaya za Mpanda, Mlele pamoja na na majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Katavi, Mpanda Mjini na Mpanda Vijijini.

No comments:

Post a Comment