13 December 2012
Maimamu watwangana makonde msikitini wakigombea uongozi
Na Sammy Kisika, Mpanda
JESHI la Polisi wilayani Mpanda, Mkoa mpya wa Katavi, linawashikilia watu wanne wanaodaiwa kuwa Maimamu wa
dini ya Kiislamu ambao wanatuhumiwa kufanya vurugu na kurushiana makonde ndani ya Msikiti wa Ijumaa Kawajensi
hivyo kusababisha ibada ishindwe kufanyika.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Dhahiri Kidavashari, alisema chanzo cha ugomvi huo ni Maimamu hao kugombea umiliki wa msikiti na kuongoza ibada.
Alisema hali hiyo ilisababisha vurugu na kuvuruga taratibu zote
za swala ya Ijumaa iliyokuwa ifanyike msikitini hapo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bw. Juma Mazomba (32), Bw. Ibrahimu Rashid (42), Bw. Mussa Hamis (27) na Bw. Husein Omary (32), ambao wote ni wakazi wa Mtaa wa Kawajense, mjini humo.
“Hawa Maimamu walifanya vurugu hizi saa 7:15 mchana na kuacha mshangao mkubwa kwa waumini wenzao walikuwepo eneo la tukio,” alisema Kamanda Kidavashari.
Aliongeza kuwa, vurugu hizo ziligeuka kuwa uwanja wa vita baada ya Maimamu hao kuanza kurushiana makonde na kusababisha baadhi ya waumini kwenda kuchukua silaha za jadi na kurudi msikitini hapo tayari kwa vita.
“Jeshi la Polisi lilipata taarifa ya vurugu hizi, askari wetu walikwenda eneo la tukio na kufanikiwa kurudisha hali ya
amani, watuhumiwa bado tunaendelea kuwashikilia kwa ajili
ya mahojiano na watafikishwa mahakamani wakati wowote
baada ya uchunguzi kukamilika,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment